Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) wamesaini Mkataba wa Makubaliano kwa lengo la kuunganisha nguvu ya pamoja ili kutatua changamoto ya biashara hususan masoko inayowakumba wananchi ikiwemo wanaushirika ambao kwa kiasi kikubwa ni wakulima.

Makubaliano hayo yametiwa saini  Machi 23, 2022 Jijini Dodoma na Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, DKt. Benson Ndiege, na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania, Latifa M. Khamis.

Dkt. Ndiege amesema kutekelezwa kwa makubaliano haya kutaviwezesha Vyama vya Ushirika na Wanaushirika kuwa na uwezo wa kuzalisha kwa tija kulingana na mahitaji ya Soko, kutangaza Bidhaa na Mazao wanayozalisha na kufikia Masoko ya uhakika na endelevu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania, amesema ushirikiano kati ya TanTrade na TCDC utawanufaisha wakulima na Wanaushirika kupata masoko ya ndani na nje ya nchi kwa bidhaa wanazozalisha.

 Makubuliano baina ya TCDC na TanTrade yanahusisha maeneo yafuatayo: Kutoa elimu na mafunzo ya kibiashara na masoko kwa viongozi, watendaji na wanachama wa ushirika; kuhamasisha makundi mbalimbali ya wananchi kuunda Vyama vya Ushirika; Kuhamasisha Vyama vya Ushirika kushiriki katika  maeonesho mbalimbali ya kibiashara ndani na nje ya nchi; Kuratibu ziara na makongamano mbalimbali ya kibiashara kwa kushirikiana na vyama vya ushirika; Kuhamasisha na kuhimiza uwekezaji katika kuongeza thamani mazao na bidhaa za Tanzania; na Kubadilishana taarifa mbalimbali kuhusu uzalishaji, usafirishaji, masoko na takwimu za mauzo.