Ofisi ya Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Shinyanga imeanza utekelezaji wa Program ya mafunzo kwa vitendo yanatolewa kwa watendaji wa Vyama vya Ushirika vinavyojishughulisha na kilimo cha Pamba.
Mafunzo hayo yamefunguliwa tarehe 18/1//2022 na Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Prof. Siza Tumbo, ambaye amepongeza Ofisi ya Mrajis Msaidizi Mkoa kwa hatua hiyo ya kutekeleza Mpango wa mafunzo kwa vitendo kwa Watendaji wa AMCOS 174 za Pamba.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga amewataka watendaji hao kupokea mafunzo hayo na kuhakikisha kile wanachojifunza wanakwenda kukifanyia kazi.
Katika ufunguzi huo Katibu Tawala ameeleza njia pekee ya kuondoa Hati zisizolidhisha ni kwa kuwapatia mafunzo Watendaji ambayo yanapaswa kuwa endelevu na kuhakikisha kuwepo na utaratibu wa ufuatiliaji wa karibu ili kujiridhisha na kile wanachokifanya watendaji baada ya mafunzo.
"Kuendelea kuwepo kwa Hati chafu sio suala la wizi bali ni uandishi mbovu ama kukosekana kwa nyaraka ambazo zinawez kupelekea dosari kwa Mkaguzi wa Nje," amesisitiza Prof. Tumbo.
Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Shinyanga, Hilda Boniphace, amemshukuru Mgeni Rasmi kwa kutoa uzoefu mkubwa wa maeneo muhimu na kumhakikshia kuwa maelekezo aliyoyatoa wameyapokea na watakwenda kuyafanyia kazi yeye pamoja na timu yake nzima ya Kamati ya Elimu ya Mkoa ambayo pia Mrajis Msaidizi ndiye Mwenyekiti wa Kamati hiyo.
Mrajis Msaidizi amesema kuwa timu ya Wakaguzi kutoka COASCO na Ofisi yake kwa kushirikiana na Mratibu wa Mafunzo Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) itakuwepo mkoani Shinyanga kwa siku tatu kwaajili ya kutoa mafunzo hayo kwa vitendo.
"Ninamshukuru sana Mkurugenzi Mkuu Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) kwa kuweka nguvu na kuonesha ushirikiano mkubwa ili kuhakikisha Watendaji wa Vyama hivi wanapatiwa mafunzo stahiki; ninashukuru ushirikiano uliopo kati ya TCDC, MoCU na COASCO," amesema Mrajis Msaidizi.
Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Shinyanga amesema kuwa mafunzo haya yanafanyika kwa vitendo ambapo Watendaji wa AMCOS za Pamba wamegawanywa katika vituo vinne vya kujifunzia. Kwa maana ya Shinyanga vituo viwili na Kahama vituo viwili.
"Lengo la mafunzo haya ni kuimarisha uandishi na utunzaji wa kumbukumbu ambao mara nyingi umekua ukisababisha kuwepo kwa Hati chafu. Hivyo Kamati ya elimu ya Mkoa ambayo inaratibu mafunzo tumekaa pamoja na kukubaliana ya kuwa tunahakikisha watendaji wetu wanabadilika hata na wao wenyenye kujenga utaratibu wa kufanya maingizo kwenye vitabu vyao vya fedha," amesema Hilda Boniphace.
Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Shinyanga amekiri kuwepo kwa Watendaji wenye umri mkubwa ambao hata ujifunzaji wao unakua mgumu hivyo ametoa wito kwa vyama kuhakikisha wanaajiri wasaidizi wa hawa watendaji wenye umri mkubwa ili waendelee kuwapa uzoefu wa kazi na baada ya muda vijana waweze kuendelea na majukumu haya.
Matarajio ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika ni kuhakikisha tunapunguza ama kuondoa Hati chafu kwenye Vyama vya Ushirika, kuimariaha udhibiti na usimamizi kuanzia ngazi ya chama cha msingi hadi vyama vya upili," amesema Mrajis Msaidizi, Hilda Boniphace.