Serikali imesema imedhamiria kuimarisha na kuendeleza azma yake ya kuimarisha, kusimamia na kuendeleza Sekta ya Ushirika nchini kwa lengo la kuondoa umaskini na kujenga uchumi imara wa Wananchi.

Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Hamis Ulega ameyasema hayo wakati wa Ufunguzi wa Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Juni 27, 2023 katika Viwanja vya Nanenane Ipuli Mkoani Tabora. 

Naibu Waziri amesema Serikali ina azma ya kuimarisha Ushirika kutokana na jitihada mbalimbali zinazoendelea ikiwemo kuimarisha na kukamilisha kanzidata na kusajili  Wakulima nchini ili taarifa hizo ziweze kusaidia katika usimamizi wa Ushirika, usambazaji wa pembejeo na Viwatilifu kwa lengo la kuongeza uzalishaji na hatimaye kukuza masoko kupitia Ushirika.

“Sote tunatambua mchango wa sekta ndogo ya ushirika katika nchi yetu hasa katika kuleta maendeleo na kukuza uchumi wa nchi. Nipende kusema kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua kwamba, ushirika unasaidia watanzania hasa wenye kipato cha chini katika kukabiliana na umasikini” alisema

Aidha, amekitaka Chuo cha Ushirika Moshi (MoCU) kuendelea kutoa mafunzo ya Ushirika kwa Wanaushirika, Wadau na Umma ili Wananchi wengi waweze kuelewa Ushirika, kutambua fursa za kiuchumi zilizopo katika Sekta ya Ushirika na kuzitumia kuondoa umaskini.

 Aidha, amesema kutokana na takwimu zilizotolewa na Shirikisho la Vyama vya Ushirika (TFC) kuonesha idadi ya wanachama wa Vyama vya Ushirika imeongezeka kutoka wanachama 6,965,272 Desemba, 2021 hadi 8,358,326 kufikia Machi, 2023. Ongezeko hilo limetokana na uhamasishaji kuhusu umuhimu wa kujiunga na ushirika. Hivyo, suala kubwa ambalo Serikali inalisisitiza ni kuhakikisha wakulima, wafugaji na wavuvi wengi wanajiunga kwenye vyama vya ushirika. 

Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Irene Madeje kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamisheni Abdulmajid Nsekela amesema miongoni mwa vipaumbele vya kuimarisha Ushirika vya Tume ni pamoja na kuimarisha matumizi ya Mifumo ya TEHAMA katika usimamizi na uendeshaji wa Vyama hasa kupitia Mfumo wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika unaosimamiwa na Tume.

Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege amesema Tume imeendelea kusimamia Sekta hiyo kwa kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuimarisha kaguzi katika Vyama, kuvunja Bodi za Ushirika pale inapohitajika, kutoa mafunzo na kuhamasisha uanzishaji wa Vyama, pamoja na kuhamasisha Amcos kuanzisha SACCOS.

Ufunguzi huo umehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wakiwemo Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Tabora, Mwakilishi wa Mrajis wa Vyama vya Ushirika Zanzibar Zainab Hassan, Kamisheni ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Wanaushirika pamoja na Wadau wa Ushirika. Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Ushirika 2023 ni “Ushirika kwa Maendeleo Endelev