Dhamira ya Serikali ni kutumia mfumo wa ushirika katika kuwewezesha wananchi kiuchumi na kuchangia ipasavyo katika ustawi wao na wa Taifa kwa ujumla. 

Kazi kubwa ya Serikali ni kuhakikisha Ushirika unahamasishwa miongoni mwa watanzania na kusimamiwa kwa mujibu wa sheria ili kuwalinda na kuwanufaisha Wanaushirika. 

Katika mwaka 2021/22, vipaumbele vya utekelezaji vilikuwa ni kuimarisha ukaguzi na usimamizi wa Vyama vya Ushirika, kuratibu uhamasishaji, Utafiti na utoaji wa elimu ya maendeleo ya Ushirika, kuimarisha masoko, uwekezaji na uwezeshaji wananchi kiuchumi. 

Kuongezeka kwa uwekezaji katika Vyama vya Ushirika kumesababisha ongezeko la ajira kutoka 100,100 mwaka 2020/2021 hadi 146,555 mwaka 2021/2022. Kati ya ajira zilizopatikana, za kudumu ni 31,819, za mkataba ni 28,990 na za msimu ni 85,746. 

Katika mwaka wa fedha 2022/23, Tume imepanga kutekeleza yafuatayo:

 Kuratibu uanzishwaji wa Benki ya Taifa ya Ushirika ili kuchochea maendeleo ya Ushirika nchini;

Kufanya uthamini wa mali zinazomilikiwa na Vyama vya Ushirika kwa lengo la kutambua thamani halisi ya soko ya mali hizo na hivyo kuviwezesha Vyama kufanya uwekezaji wenye tija;

Kuanzisha Mfuko wa Bima ya Akiba na Amana za SACCOS utakaotumika kama kinga ya akiba na amana za wanachama wa SACCOS ambao SACCOS zao zitashindwa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria;

Kuimarisha udhibiti na usimamizi wa Vyama vya Ushirika kwa kutoa mafunzo kwa maafisa Ushirika 226, Kukagua vyama vyote, na kuendelea kununua vitendea kazi na kununua magari kwa ajili ya kuongeza tija kwa maafisa ushirika;

Kuanza matumizi ya Mfumo wa Usimamizi na Ukaguzi wa Vyama vya Ushirika na  kuhamasisha, kuratibu na kusimamia ujenzi na ufufuaji wa viwanda ili kuongeza thamani ya mazao; 

Kuratibu na kuhamasisha ujenzi wa maghala ya mazao ya kilimo ili kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno, kuongeza thamani ya mazao na kuimarisha mfumo wa minada ya mazao yanayozalishwa na wananchi;

Kutengeneza utaratibu wa uwezeshwaji vyama vya Ushirika (cooperative facilitation scheme) ili kuongeza ufanisi wa vyama vya Ushirika; na

Kuimarisha zaidi matumizi ya Vyombo vya Habari (TV, Redio na Mitandao ya Kijamii) katika uhamasishaji wa wananchi kujiunga na Vyama vya Ushirika na manufaa ya kuwa katika Ushirika.