Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt.Benson Ndiege, amewataka watumishi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika kufanya kazi kwa weledi na kwa kuzingatia sheria,kanuni na taratibu za kazi.

Dkt.Ndiege ameyasema hayo wakati wa kikao cha watumishi wote wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika wa makao makuu na wawakilishi wa watumishi wa Tume kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara kilichofanyika tarehe 21/12/2022 JIjini Dodoma.

"Kuweni waadilifu na msijihusishe na Rushwa na kufuata taratibu za Utumishi wa Umma,tuheshimiane,viongozi hamtakiwi kuwadharau,watumishi wenu,pia tuendelee kutoa huduma bora kwa Wanaushirika na Wananchi kwa ujumla ili kujenga Ushirika wenye tija kwa maendeleo ya Taifa letu," alisema Ndiege.

Aidha, Dkt Ndiege amesisitiza kuwa Watumishi waendelee kuitangaza Tume ya Maendeleo ya Ushirika na katika kuitangaza wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii na kazi hizo zionekane kwa watu mbalimbali na Wanaushirika ili kuweza kufikia malengo tuliyojiwekea.

"Katika kujitangaza kama Tume ya Maendeleo ya Ushirika tunatakiwa kufanya kazi kwa bidii na kuchukua hatua ili walioko nje ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika waone nini kinafanyika,kujitangaza tu kupitia Vyombo vya Habari pekee haisaidii lakini kupitia kazi nzuri zinazofanyika na watumishi wa Tume na Wanaushirika tutakuwa tumeutangaza Ushirika kwa kiasi kikubwa," amesema Dkt Ndiege.

Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika ameahidi kuendelea kutatua changamoto mbalimbali ambazo zinajitokeza katika utendaji wa kazi ikiwemo kuboresha maslahi ya watumishi na kuongeza vitendea kazi.

Aidha, Mrajis amewataka watumishi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika kujiendeleza kielimu ili kuweza kuendana na hali halisi ya uhitaji wa Teknolojia na mbinu za kiutendaji zinazohitaji watumishi wenye elimu na weledi zaidi.

"Kujiendeleza kielimu ni fursa muhimu kwa maendeleo ya mtu mmojammoja na Taifa kwa ujumla, maana ukishajiendeleza kielimu unaweza ukapata nafasi mbalimbali za kiutumishi, lakini usipojiendeleza nafasi zinaweza zikatokea na zikakupita na kuchukuliwa na watu wengine wenye sifa na waliofikia ngazi za kielimu zinazohitajika" amesema Dkt. Ndiege.