Makabidhiano ya Tsh 443,997,550 kutoka TFC kwenda KBCL yaliyoshuhudiwa na Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe

Waziri wa kilimo, Mheshimiwa Hussein Bashe, amevitaka Vyama vya Ushirika  kuanzisha  Benki ya Taifa ya Ushirika Tanzania (National Cooperative Bank - NCB) itakayomilikiwa na Wanaushirika wenyewe. 

Mheshimiwa Bashe alikuwa akizungumza na Viongozi wa Vyama vya Ushirika,  Machi 17, 2022 Jijini Dodoma ambapo amesema Benki hiyo itaanza na kianzio cha Shilingi Bilioni 15 na  hadi sasa kuna Shilingi Bilioni 3.3, ambapo Shilingi 443,997,550 zimekabidhiwa leo kwa Benki ya Ushirika  ya Kilimanjaro (KCBL) kutoka Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC)  zilizochangwa na baadhi ya  Vyama vya Ushirika nchini.

Waziri wa Kilimo amesema kuwa Benki ya Ushirika ya Taifa itakuwa na Makao yake Makuu Jijini Dodoma na itakuwa na Matawi nchi nzima kupitia Benki ya CRDB ambapo itavihudumia Vyama Vyote vya Ushirika vitakavyochangia Mtaji wa kuanzisha Benki hiyo.

Aidha, Waziri Bashe amevitaka Vyama Vikuu vinavyosimamia Mazao ya Makuu ya kibiashara ya Pamba, Korosho, Kahawa na Tumbaku kusimamia ukusanyaji wa makato ya Wakulima yatakayowezesha kukuza  Mtaji wa kuanzisha Benki hiyo kwa haraka; na amesema kila Mkulima  atakayechangia atapewa Cheti cha umiliki wa Hisa za Benki hiyo.

Kuanzishwa kwa Benki ya Taifa ya Ushirika  kutaviwezesha Vyama vya Ushirika  kufanya Biashara, kupata Mikopo yenye Riba nafuu na kuviwezesha kujiendesha kibiashara na kuwalinda Wanaushirika wakiwemo Wakulima, kutokunyonywa na Taasisi za Fedha zinazotoa Mikopo yenye Riba kubwa.