Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Antony Mavunde, amesema kutokana na Tafiti zinazofanyika kwenye Sekta ya Ushirika, sasa Ushirika unaenda kuwa wa kuzalisha utajiri na sio migogoro na matatizo.

Naibu Waziri Mavunde ameyasema hayo leo tarehe 12/05/2022 kwenye ufunguzi wa Kongamano la Pili laTafiti za Ushirika lililoandaliwa na Tume ya maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu Cha Ushirika Moshi (MoCU).

Mhe. Naibu Waziri amewataka Wanaushirika  kwenda kubadili  picha na mtazamo wa Ushirika na si kubaki kukazana na yale yale mambo mabaya kila siku ambayo yameendelea kuurudisha nyuma Ushirika.

"Ushirika huu una uwezo kuwa na mchango mkubwa kwenye ustawi wa taifa letu la Tanzania, tunauweza kupiga hatua kwa kujiunga kwenye Ushirika," amesema Mheshimiwa Mavunde.

"Ukiangalia  fursa mbalimbali zilizopo nchini, kama upatikanaji mafuta ya kula; Kuna uhitaji wa Tani Laki Sita na elfu hamsini kwa mwaka na uwezo wa ndani wa kuzalisha ni Tani laki mbili na tisini elfu tu, inailazimu Serikali kuagiza mafuta ya nje  yenye thamani ya billion 474. Kwahiyo kupitia Kongamano hili twendeni tuje  na suluisho kuisaidia Serikali," amesema Mhe. Mavunde

Aidha, amewapongeza Wanaushirika kwa kuafiki na kuanzisa Mfuko kwa ajili ya Tafiti, na kuridhia kuanzishwa kwa Benki ya Taifa ya Ushirika.

Awali, Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini (TCDC), Dkt. Benson Ndiege amesema, kongamano hilo ni muhimu katika kuibua changamoto za Ushirika na kuzitafutia ufumbuzi.

“Tunachotakiwa hapa ni kuibua changamoto na kuziweka kwenye utekelezaji wa mwaka unaokuja.” amesema Dkt. Ndiege.

Akitoa maelezo ya kongamano hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya kongamano hilo, Dkt. Edmund Zakayo, amesema wameamua kufanya makongamano ya tafiti za Ushirika kutokana na tafiti nyingi kutokuwa na tija kwa kuwa zinaandaliwa na kuandikwa kwa lugha ya kiingereza, ambayo siyo rafiki kwa baadhi ya Wanaushirika.

Amesema, hali hiyo imefanya tafiti hizo kubaki kwenye makaratasi kutokana na lugha inayotumika katika kuyaandaa na kutokusambazwa kwa walengwa.

“Kutokana na hali hiyo ikaonekana umuhimu wa kuandaa kongamano la kwanza la tafiti za Ushirika na hatimaye kuazimia kuwa na kongamano kila mwaka ili tuweze kupata fursa ya kujadiliana matokeo ya tafiti na namna ya kutatua changamoto zilizopo katika Sekta ya Ushirika.” amesema Dkt. Zakayo.