Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Ushirika & Umwagiliaji Dkt.Stephen Nindi ameitaka Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) kuimarisha usimamizi wa Vyama vya Ushirika na Mifumo ya Kidigitali ili kuongeza tija na uchumi kupitia Ushirika.
Dkt.Nindi amesema hayo Aprili 17, 2025 wakati wa kikao na Watumishi wa Tume, kilichofanyika Jijini Dodoma, ambapo mesema Tume inapoendelea kusimamia Vyama vya Ushirika mifumo ya uzalishaji mali itaimarika.
Aidha, ametoa wito rasilimali za Vyama kusimamiwa vizuri ikiwa ni pamoja na ardhi, mashamba, viwanda, maghala ili ziongeze tija na Uchumi wa Vyama.
Sambamba na hilo ameeleza kuwa Benki ya Ushirika inayotarajiwa kuzinduliwa Aprili 28, 2025 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan itaongeza msukumo wa kiuchumi kwa Vyama hasa Vyama vitakapokuwa vina mifumo imara ya uendeshaji.
Mrajis na Mtendaji Mkuu wa TCDC, Dkt.Benson Ndiege, amesema Tume itaendelea kusimamia Vyama kwa kuzingatia Vipaumbele vya Tume ikiwemo uhamasishaji wa uanzishaji wa Benki ya Ushirika.
Pamoja na mambo mengine, wataalamu mbalimbali akiwemo Dkt. Chriss Mauki walitoa mada ya masuala ya Afya ya Akili, Utunzaji wa Mazingira, Nishati safi ya Kupikia, Lishe na ulaji unaofaa ili kuwaongezea maarifa Watumishi katika utekelezaji majukumu na maisha yao.