TUME YA USHIRIKA NA BENKI YA NMB ZAINGIA MAKUBALIANO UJENZI WA MAGHALA KWENYE VYAMA VYA USHIRIKA

Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) imeingia Randama ya Makubaliano na Benki ya NMB kushirikiana katika kuwezesha ujenzi wa maghala kwenye Vyama vya Ushirika nchini.

Makubaliano haya yametiwa saini Jijini Dodoma leo, 15/06/2022 na Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, Dkt. Benson Ndiege, na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Juma Kimori ambapo wamesema ushirikiano huo una lengo la kuhakikisha maghala yanajengwa kwenye Vyama vya Ushirika nchi nzima.

“Matarajio tuliyonayo ni kutatua changamoto ya kukosekana kwa maghala yenye ubora katika Vyama vya Ushirika vya Msingi na Vyama Vikuu kwa mazao ya Kimkakati na  maghala haya  yatatumika pia kwenye mazao mengine yanayolimwa na wakulima katika maneo yao,” amesema Dkt. Ndiege.

Aidha, Dkt. Ndiege ametoa wito kwa Vyama vya Ushirika: kushirikiana na benki ya NMB na TCDC katika kutoa taarifa za uzalishaji ili kubaini ukubwa wa ghala unaohitajika; kushirikiana kwa Benki ya NMB na TCDC katika utekelezaji wa shughuli za Randama ya Makubaliano ili kufanikisha  ujenzi wa Ghala; na Kutunza maghala yatakayojengwa au kuboreshwa kupitia makubaliano yaliyofikiwa.