TCDC yatoa msaada kwa watoto wenye mahitaji maalum wa kijiji cha matumaini, Dodoma

KATIKA kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani, Tume  ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania  (TCDC) imetoa msaada wa chakula, mafuta, Pempers na sukari  kwa watoto wanaoishi na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi katika Kituo cha Matumaini Jijini hapa huku ukitolewa wito kwa watanzania kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalum.

Akizungumza leo Machi 8,2022, Jijini Dodoma wakati wa utoaji wa msaada huo, Afisa Utawala kutoka (TCDC), Joyce Kato amesema wamechagua kupeleka msaada huo katika  kijiji cha Matumaini kutokana na mahitaji ya watoto hao kuwa makubwa.

“Tumechagua kijiji cha Matumaini kwa kuwa sisi  kila tunaposhiriki maadhimisho  tunachagua kituo cha kwenda kutoa msaada,  mwaka jana tulienda Buigiri lakini sasa hivi tumechagua Matumaini kwa sababu hawa  wana mahitaji sana,” amesema.

Amesema nia ya TCDC  ni kuwasaidia watoto kwa kuwa wamekuwa wakipata changamoto mbalimbali.

“Wito wetu  kwa Taasisi zingine tujitoe tukipata uwezo wa kusaidia tusaidie kwa sababu  hawa  watoto wanatuhitaji sisi,” amesema.

Naye, Mjumbe wa Kamati ya  TUGHE  wanawake,  Tatu Mwenda amesema kwa mwaka huu waliandaa  maadhimisho haya ambapo lengo ni kusheherekea na wanawake ambapo amedai walipata ushirikiano mkubwa kutoka kwa mwajiri kuanzia katika mavazi,mpaka misaada.

“Lengo kubwa ni kutoa msaada kwa watoto wale tumepeleka pampers za watoto,mchele,maharage,sabuni sukari tumetumia milioni moja ambayo Sister alituomba lakini sisi kama wazazi tumeona kuna vifaa vina umuhimu,”amesema.

Mwenda ametoa wito  kwa Serikali,Makampuni na Taasisi  kuendelea kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalum huku akiupongeza uongozi wa TCDC   kwa kujitolea kuwasaidia watoto.

Kwa upande wake,Sister wa Kituo hicho,amesema wamekuwa wakikutana na changamoto mbalimbali lakini wamekuwa wakizitatua kwa baadhi ya watu,taasisi na Serikali kuwasaidia

Amesema watoto hawa wanaishi vizuri kwa sababu wanatumia dawa na wengine tayari wamemaliza chuo na wana kazi na  hakuna kukata tamaa licha ya kwamba watoto hao ni  yatima lakini wanaishi kifamilia.

“Wengine wenye moyo wa kujitolea wanakuja mtu na mme wake ambao pengine wameishakuwa na watoto wakubwa wanalea wale watoto yatima mnampa nyumba mnamgawia na watoto ili wapate malezi ya baba na mama na wanaenda mara moja kwa mwezi.

“Kuna wengine wamekaa sana kuna wengine wana  miaka 16 tangu wamekuja na familia yao ambapo familia yako unaiacha nyumbani ili kuwalea watoto hao,”amesema.

Amesema watoto wanaioshi katika kituo hicho wapo 147 ukiacha wale ambao wapo shule za Sekondari na Vyuo.

Amesema kuna mtoto wa siku 18 ambaye aliletwa katika kituo hicho mara baada ya mama yake kupata kichaa na wamekuwa wakimuhudumia vizuri.

“Na  mdogo kabisa ana siku 18 tangu amezaliwa ameletwa akiwa na siku nane, Mama yake anashida  anakichaa alimtupa hivyo ndugu walishindwa jinsi ya kumsaidia wakaona Mama wampeleke Mirembe na mtoto wamlete hapa sisi hatuwezi kukataa,”amesema.