Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) na Bodi ya Sukari Tanzania (TSB) zimesimamia zoezi la Ugawaji wa Mali na Madeni na usainishwaji Hati za makubaliano  kwa AMCOS za Miwa bonde la Kilombero baada ya kupangwa kijiografia.

Zoezi hilo limefanyika tarehe 25/04/2023 Ruaha Kidatu katika Halmashauri ya Kilombero na kukamilika baada kikao kazi kilichofanyika na kubaini kuwepo kwa malalamiko yaliyokuwa yakitolewa na wadau wa Tasnia ya sukari bonde na Vijiji na kata kwa upande wa Kilombero na Kilosa ili kuona hali halisi ya mpangilio wa mashamba na wakulima wa miwa.

Akiongea wakati wa ufunguzi wa zoezi hilo Naibu Mrajis wa Vyama Vya Ushirika (Usimamizi na Udhibiti) Collins Nyakunga, amesema kuwa, changamoto zilizokuwepo kwa wakulima kwa sasa hazitakuwepo tena kwani maeneo yote yameshapangwa kijiografia na hivyo kuwarahisishia wakulima kuweza kufanya maamuzi kwa pamoja.

"Ndugu zangu jambo lililofanyika ni la msingi sana litaturahisishia sana wakati wa kuvuna, kusafirisha na kuwahudumia wakulima kwa wakati na kutatua changamoto kama za moto katika mashamba ya miwa," amesema Nyakunga.

Naibu Mrajis ameongeza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Ushirika Na 6 ya mwaka 2013 kifungu namba 98, inaamriwa kuwa Vyama vyote vya Ushirika ambavyo havijiwezi na havifanyi vizuri tunavihamasisha na kuunda Vyama vya Ushirika vilivyo imara na kuwa na uwezo wa kuzalisha kwa wingi.

Naye Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika wa Mkoa wa Morogoro,  Keneth Shemdoe amesema kuwa baada ya zoezi hilo kukamilika Vyama vinaenda kujiendesha kibiashara ambapo kila Chama kitakwenda kusimamia misingi ya kijiografia iliyotumika katika Ugawaji wa Mali za vyama hivyo.

"Mali, fedha na samani zote za Vyama vilivyogawanywa leo zimegawanywa kiusawa kwa asilimia 100 kwa kila Chama kwa kuzingatia kiwango cha hisa zilizokuwepo kwa kila Chama cha Ushirika," amesema Shemdoe.

Zoezi hilo pia litasaidia kuongeza uwazi, kusogeza karibu huduma za uvunaji, kutambua maeneo yaliyo mabondeni na kuwapa kipaumbele katika uvunaji, kupunguza kuvuniwa kwa upendeleo, kukopesheka kirahisi kwenye taasisi za kibenk,kuwezesha zoezi la usajili kwa wakulima, kupunguza ajali za moto, kurahisisha miundo mbinu ya barabara za mashambani.

 Zoezi hilo limefanikiwa kupanga Vyama kijiografia kutoka AMCOS 20 hadi 17 ambapo kwa upande wa Wilaya ya Kilombero (K1) ni AMCOS 8 na kwa upande wa Wilaya ya Kilosa (K2) ni AMCOS 9.