Waziri Mkuu Aagiza Ushirika wa Zabibu Kuimarishwa.

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amevitaka Vyama vya Ushirika vya Kilimo cha zabibu kuimaimarishwa ili kuongeza uzalishaji na tija itakayochochea maendeleo ya uchumi wa Viwanda nchini.

Ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa zao la zabibu mkoani Dodoma Julai 6, 2020 waliokutana kwa lengo la kujadili namna bora ya kuendeleza zao hilo kwa kuangalia changamoto, fursa zilizopo katika kilimo cha zabibu na kuweka mikakati ya pamoja.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Waziri Mkuu amesema ni muhimu vyama vya Ushirika hasa vilivyopo mkoani Dodoma kwenye uzalishaji mkubwa wa zao hilo kuzingatia taratibu sahihi za kilimo hicho kwa kusaidiana na maafisa ugani wa maeneo yao, kuanzisha vitalu vya miche bora katika maeneo ya mashamba ya Ushirika pamoja na kuzingatia masuala ya utawala bora katika uendeshaji wa Vyama hivyo.

“Ni lazima vyama vya Ushirika vihakikishe vinaanzisha vitalu vya miche katika mashamba ya Ushirika na niwaombe viongozi pamoja na watendaji wa Serikali wote katika Sekta ya Ushirika kusimamia kilimo hiki ili kupanua kilimo cha zabibu na kuongeza uzalishaji ambao kwa sasa bado ni mdogo,” alisema Waziri Mkuu

Aidha, Waziri Mkuu ameagiza Ushirika kuwa na kanzidata itayorahisisha utambuzi wa wakulima wa zabibu kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma za ugani, usambazaji wa pembejeo pamoja na masuala ya masoko.

“Kanzidata itasaidia sana kujua wakulima wetu kwenye vyama vya Ushirika wako wapi, wana mashamba ya ukubwa gani na taarifa zingine kumhusu mkulima ili iturahisishie tutakapohitaji kupanga mikakati ya huduma kwa wakulima kwa usahihi zaidi,” alisisitiza

Akielezea mikakati ya Serikali katika kuimarisha ushirika Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali itaendelea na jitihada za kulinda bidhaa zinazotengenezwa na viwanda vya ndani ya nchi ikiwa ni hatua ya kuendelea kuhakikisha bidhaa hizo zinapata soko kubwa. Akiongeza kwa kutoa wito kwa wamiliki wa Viwanda vya kuchakata zabibu kuendeleza uzalishaji wa bidhaa hizo ambazo bado uhitaji wa soko ni mkubwa ndani nan je ya nchi.

Akiongea kwa niaba ya wanaushirika wa Chama cha Wazamah Hombolo Stanslaus Nzaga amesema baadhi ya masuala ambayo bado ni changamoto katika kilimo cha zabibu ni taratibu ngumu za upatikanaji wa mitaji ya kuendesha kilimo hicho, uchakavu wa miundombinu hasa ya umwagiliaji na barabara na hivyo kupendekeza kuanza kufikiria kuwepo kwa chombo maalum cha kusimamia zao hili hapa nchini.

Mkutano huo ulihudhuriwa na wadau mbalimbali ikiwemo wamiliki wa viwanda, wakulima, wanaushirika, watendaji wa Serikali, wabunge, taasisi za kifedha, mashirika ya Utafiti wa Kilimo pamoja na wahamasishaji wa zao hilo kutoka maeneo mbalimbali. Hii ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa Kampeni ya uhamasishaji wa kilimo na uzalishaji wa zabibu nchini.