Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe, amesema Bima ya Mazao itasaidia Wakulima kuondokana na Vihatarishi  kabla na Baada ya kuvuna mazao ya Wakulima ili  kuzalisha kwa tija na kuongeza kipato zaidi.

Amesema hayo katika kikao cha kujadili mpango wa Maalum wa Bima ya zao la Tumbaku na wadau, Vyama vya Ushirika vya mkoa wa Tabora pamoja na wataalamu wa zao la Tumbaku, Januari 24, 2025 Jijini Dodoma.    

Waziri Bashe amesema Mkulima huingia hasara kutokana na vihatarishi vya aina mbalimbali kama vile ukame, Mvua za mawe, mafuriko, magonjwa ya mazao. Hivyo, Bima itasaidia Wakulima kulima kwa tija na kuzalisha mazao mengi.

Amewataka Wataalamu kujadili kwa kina na kuweka mapendekezo dhabiti na kuja na Mpango wa Bima kwa Zao la Tumbaku utaweza kutumika kwa mazao mengine baadae.

Ameongeza kuwa ni muhimu Wanunuzi na Wadau wengine washirikishwe ili kupata Bima itakayokidhi mahitaji ya Wakulima.

Aidha, ameonya baadhi ya Wakulima wanaotorosha Tumbaku kuacha kufanya hivyo, kwani kunadhoofisha juhudi za kukuza mnyororo wa fedha hasa pale makato ya Mikopo ya wakulima yanapohitajika kufanyika na  Mkulima kuuza Tumbaku kwingineko tofauti na utaratibu.

Washiriki wa kikao hicho ni pamoja na Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Tabora, Vyama vya Ushirika, Makampuni ya Bima, Mabenki,  Wanunuzi wa Tumbaku pamoja na Bodi ya Tumbaku.