Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Bashe akifungua zoezi la ugawanji mbolea kwa wakulima Simuyu

Waziri wa Kilimo Mhe. Husein Bashe amemtaka Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Simiyu (SIMCU ) Lazaro Walwa kuhakikisha anajua uhitaji wa idadi ya mbegu zitakazowatosheleza katika kilimo msimu huu.

Amesema baada ya kujua uhitaji huo wanapaswa kuhakikisha mbegu hizo zinawafikia walengwa kwa kushirikiana  na  Bodi ya Pamba Mkoa wa Simiyu.

Waziri wa Kilimo alikuwa akizungumza katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Chakula Duniani  jana tarehe 16 Oktoba 2022  alipotembelea banda la Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania.

Awali, Mhe. Bashe alielezwa hatua iliyofikiwa katika ufufuaji wa kiwanda cha uchakataji Pamba ambapo unaitaji Shilingi Bilioni 1.4  na hatua iliyopo sasa ni hatua ya awali.

"Nyie kama Chama mnachojiweza na ninaimani mtafanikiwa hivyo anzeni kutumia pesa mnazopata za ushuru mtapokwamia basi Wizara nitawasaidia kuanzia hapo," alisema Mhe. Bashe.

Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Simiyu, Lazaro Walwa, amemuomba Waziri wa Kilimo kuwasaidia kuboresha mfumo wa ukusanyaji mapato katika vyama usiwe wa kukatwa ushuru kwa pesa taslimu kwani hiyo inasababisha upotevu wa fedha nying hivyo wameomba  uwepo mfumo wa kidigital ili kurahisisha ukusanyaji wa ushuru.

MWISHO