Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Collins Nyakunga, ametoa wito kwa Watumishi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) kuzingatia Kanuni za Afya kwa lengo la kujikinga na maambukizi ya VVU/UKIMWI pamoja na magonjwa yasiyoambukiza ili kutunza nguvu kazi pamoja na ustawi wa jamii.

Wito huo umetolewa leo Aprili 05, 2023 wakati wa ufunguzi wa mafunzo kuhusu Maambukizi ya VVU/UKIMWI na Magonjwa yasiyoambukiza kwa Watumishi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika yaliyotolewa Jijini Dodoma.

Akifungua mafunzo hayo Naibu Mrajis amesema mafunzo hayo ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Serikali kupitia utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa kudhibiti VVU/UKIMWI kwa lengo la kuimarisha na kuendeleza ufanisi katika Utumishi wa Umma.

Sambamba na Mafunzo hayo watumishi wa Tume wamepata fursa ya kupata elimu ya utunzaji na kanuni bora za afya, ushirikiano mahala pa kazi, pamoja na zoezi la upimaji wa afya lililofanyika kwa lengo la kusaidia watumishi kujua vyema afya zao na kuchukua hatua sahihi.  

Mafunzo hayo yameratibiwa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika na kuwezeshwa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kupitia Mkurugenzi Msaidizi- Anuai za Jamii, Mwanaamani Juma Mtoo, aliyeambatana na Dkt. Ibrahim Haule kutoka TACAIDS.