Mrajis na Mtendaji Mkuu Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Dkt Benson Ndiege, ameagiza kufutiwa leseni Watoa Huduma ambao si waaminifu wanaofanya kazi na Vyama vya Ushirika.

Dkt. Ndiege amesema Watoa Huduma ambao si waaminifu wanatakiwa kufutiwa mara moja leseni zao pale wanapokuwa wanaenda kinyume na kanuni na taratibu za Ushirika na si kusubiri mpaka wamalize muda wao ndiyo wachukuliwe hatua.

Mrajis amesema hayo leo tarehe 01/06/2023 Jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo kwa Watoa Huduma wapya 27 wakusanyaji madeni 12, TEHAMA 6, Bima 2, Huduma za Sheria 3 na Ushauri wa Biashara 4.

Aidha, Dkt Ndiege amesema wapo watoa huduma wenye nia ovu na Ushirika kwasababu wanaingia katika kazi hiyo kwa lengo la kujinufaisha wao na wanasahau kama wao ndiyo daraja la kumaliza chagamoto katika Ushirika na si chanzo cha migogoro.

“Ushirika si chaka la watu wasio na maadili  acheni kujiingiza kwenye Ushirika kwa lengo la kutajirika, fanyeni kazi kwa kufuata taratibu na miongozo ya Ushirika kwa maslahi ya wanaushirika hapo Ushirika utafika mbali,” amesema Dkt Ndiege.

Pia Mrajis amesema ni wajibu wa kila Mtoa Huduma kutuma taarifa ya utendaji kazi wake wa kila robo kwa TCDC, lakini wamekuwa hawatoi taarifa hizo na kusababisha kukosekana kwa takwimu za kazi zinazofanywa, hivyo kukosa sifa za kuendelea kufanya kazi na Vyama vya Ushirika.

Wakati huo  huo Mtoa Huduma, Dkt Alphonce Massage, kwa niaba ya Watoa Huduma waliohudhuria Mafunzo hayo amesema watakuwa waadilifu na watafanya kazi kwa bidi kwa kufuata miongozo na Sheria ya Vyama vya Ushirika Na. 6 ya mwaka 2013.

Pia ameishukuru TCDC kwa kuona umuhimu wa kuwaita na kuwapatia mafunzo ambayo yatawajenga katika kazi zao za kila siku na kuahidi kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na Warajis Wasaidizi wa Mikoa.