Naibu waziri wa Wizara ya Kilimo Mheshimiwa Anthony Mavunde akitoa salamu kwa wanawake waliohudhuria kongamano la wanawake lililofanyika Jijini Mwanza
Mrajis wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt Benson Ndiege akizungumza na Wanawake waliohudhuria kongamano la wanawake lililofanyika Malaika Beach Resort
Mgeni Rasmi Waziri wa Aridhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa Angelina Mabula akiongea na washiriki wa Kongamano la Wanawake liliofanyika Jijini Mwanza

Waziri wa Aridhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Dkt. Angelina Mabula, amewataka wanawake walio katika Ushirika wa Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) kuacha kuwa wanyonge badala yake wajikite kuwania nafasi za uongozi katika Vyama vya Ushirika.

Amesema  idadi ya Wanaushirika Wanawake kwenye Sekta ya Ushirika ni kubwa  lakini viongozi Wanawake kwenye Sekta hii ni ndogo sana.

Waziri Dkt. Mabula ametoa wito huo leo tarehe 16/10/2022  wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Wanawake lililofanyika  Malaika Beach Resort Jijini Mwanza litakaloambatana na  Maadhimisho ya Kimataifa ya Ushirika wa Akiba na Mikopo Duniani yatakayofanyika mkoani Mwanza kuanzia tarehe 16 hadi 20/10/2022. 

Mheshimiwa Dkt. Mabula amesema Tume ya Maendeleo ya Ushirika inatimiza majukumu yake ya Kisheria ya kuhakikisha wanaushirika Wanawake  wanapatiwa elimu na mafunzo ya Usimamizi na Uendeshaji wa Vyama vya Ushirika na umuhimu wa wanaushirika kuchukua nafasi za uongozi kwenye Vyama vyao.

Aidha, Mhe. Dkt. Mabula amewasisitiza Wanawake kupitia Ushirika kuwa waadilifu katika uchukuaji na urejeshaji Mikopo kwenye Vyama vyao kwani kutokufanya marejesho kwa wakati utadhoofisha uwezo wa kiuchumi wa Vyama vyao.

Aliendelea kuwasisitiza Wanawake kujitambua juu ya fursa zinazowazunguka, kujifunza namna ya kuzitumia vizuri katika wakati muafaka kwa Maendeleo yao kiuchumi na uimara wa Vyama vyao vya Ushirika wa Akiba na Mikopo pamoja na kuhakikisha wanaacha alama katika uongozi wao ndani ya Vyama vyao.

Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Anthony Mavunde, amewataka wanawake kujikita katika kuongeza thamani ya mazao ya kilimo kupitia Ushirika. Pia amesisitiza uanzishaji wa SACCOS kwenye AMCOS uendelee kuhamasishwa na kuhimizwa kwani utasaidia kuimarisha uwezo wa Vyama hivyo kiuchumi na kuongeza uzalishaji kwa kiwango kikubwa.

Naye Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, Dkt. Benson Ndiege, amesema Tume ya Maendeleo ya Ushirika imejipanga kuwafanya wanawake kuweza kujikwamua kiuchumi kupitia Vyama vyote vya Ushirika wa Kifedha na usio wa Kifedha.

"Hii itasaidia Wanaushirika wakinamama kujikwamua kiuchumi na kuwa na mitaji ya kutosha ambayo itawafanya waweze kutengeneza bidhaa zilizo bora ambazo zitaingia katika masoko makubwa," 

MWISHO