Naibu Mrajis - Uhamasishaji, Consolata Kiluma, ametoa wito kwa Wanawake kujitokeza kuwania Uongozi katika Vyama vya Ushirika ili kuongeza msukumo wa Maendeleo ya Ushirika.
Akiongea na Viongozi Wanawake katika Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) wakati wa Warsha maalum ya Wanawake wa Ushirika wa Akiba na Mikopo Jijini Dodoma Machi 14, 2025.
Amesema Tume ya Maendeleo ya Ushirika inaendelea kuunga Mkono jitihada za kuwawezasha Wanawake kushiriki na kutoa mchango wa kimaendeleo kupitia nafasi za Uongozi kuendesha Vyama vya Ushirika.
"Tayari Tume ilishatoa Waraka Na. 2 wa mwaka 2023 unaoelekeza theluthi moja ya Wajumbe wa Bodi kuwa Wanawake," amesema.
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake wa Ushirika wa Akiba na Mikopo, Justicia Masinde (ADE), amesema lengo la warsha hiyo ni pamoja na kujadili fursa na changamoto za wanawake ili kukuza na kuendeleza Ushirika.
Akitoa mada katika warsha hiyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), Dkt. Grace Mori, amesema kuwa Usawa wa Kijinsia unazingatia fursa sawa katika masuala ya kielimu, mafunzo, uongozi, ajira na kisiasa.
Aidha, katika warsha hiyo Shirika lisilo la Kiserikali la DSIK limezindua Programu maalum iitwayo "Wasili" kuwajengea uwezo Wanawake kuwa Viongozi bora, ubunifu pamoja na matumizi ya mifumo ya Kidijitali.
Warsha hiyo imeandaliwa na Chama Kikuu cha Ushirika wa Akiba na Mikopo - SCCULT (1992) LTD. Washiriki wametoka katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dodoma, Dar es Salaam, Kagera, Morogoro na Kilimanjaro.