Watumishi wa Idara ya Maendeleo ya Ushirika Zanzibar wamefanya ziara ya mafunzo katika Vyama vya Ushirika Mkoani Dodoma kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu Maendeleo ya Ushirika Tanzania Bara.

Katika ziara hiyo iliyofanyika leo tarehe 11 Machi 2025, Wanaushirika kutoka Zanzibar waliambatana na wenyeji wao Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) na ilihusisha kutembelea vyama vya ushirika vya Akiba na Mikopo pamoja na vya Kilimo, kikiwemo K.K.K.T Arusha Road SACCOS LTD, UDOM SACCOS LTD, CHABUMA AMCOS LTD, na BBT Chinangali AMCOS LTD.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mrajisi na Mtendaji Mkuu wa TCDC, Dkt. Benson Ndiege, amesema kuwa tukio hilo limekuwa la manufaa kwa pande zote mbili, kwani limewapa fursa ya kubadilishana mawazo na kujifunza jinsi ushirika unavyofanya kazi katika Tanzania Bara na Zanzibar.

"Tanzania ina Vyama vingi vya Ushirika vya aina mbalimbali, hivi tulivyotembelea leo ni sehemu ndogo tu, na nina imani kuwa mtarudi tena ili kujifunza zaidi kutoka kwa vyama vingine vilivyopo mikoa mingine," amesema Dkt. Ndiege.

Kwa upande wake, Naibu katibu Mkuu, Kazi na Uwezeshaji  kutoka Ofisi ya Rais Kazi Uchumi na Uwekezaji, Halima Maulid Salum, amesema kuwa ziara hiyo imewapa maarifa mapya ambayo yatasaidia kuboresha Vyama vya Ushirika Zanzibar.

"Tumepata mambo mazuri sana, lakini pia tunapenda na ninyi mfike Zanzibar kuona namna tunavyotekeleza ushirika wetu. Ushirikiano wetu utaimarisha maendeleo ya sekta hii kwa pande zote mbili," alisisitiza.

Naye Mkurugenzi wa Utumishi na Uendeshaji kutoka Ofisi ya Rais – Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Mohammed Jaffar, amesema kuwa vyama walivyotembelea ni mfano wa kuigwa, hasa kwa mchango wao katika kutoa ajira kwa wananchi.

"Mnafanya kazi kubwa kwa kutoa ajira za muda mfupi na za kudumu kwa wananchi, jambo ambalo linapunguza tatizo la ukosefu wa ajira nchini. Pia, mmeonesha uzalendo kwa kulipa kodi kutokana na ajira mnazozalisha na huduma mnazotoa," alisema Jaffar.

Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za kuboresha Sekta ya Ushirika nchini kwa kuhamasisha ushirikiano kati ya Tanzania Bara na Zanzibar ikiwemo kubadilishana uzoefu na mbinu bora za uendeshaji wa vyama vya Ushirika ushirika.