WANAUSHIRIKA JIJINI DODOMA WAJENGEWA UWEZO
Wanaushirika na wakazi wa Jiji la Dodoma wamepata fursa ya kujengewa uwezo katika maeneo mbalimbali kupitia mafunzo, maonesho pamoja na majadiliano yanayofanyika katika Viwanja vya Nyerere Square kuanzia Mei 23 hadi 24, 2024 katika Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika la Mkoa wa Dodoma.
Akiongea wakati wa ufunguzi wa Jukwaa hilo Kaimu Mrajis Msaidizi wa Mkoa wa Dodoma Octavian Bidyanguze amesema Jukwaa hilo ni mahususi kwaajili kuleta Vyama vya Ushirika pamoja ili kujifunza mada mbalimbali, kujadili fursa na changamoto za kiushirika katika utendaji kazi za Vyama, kuimarisha mshikamano na mahusiano baina ya vyama.
Baadhi ya mada na majadiliano kwenye Jukwaa hilo yalijikita katika masuala ya Sheria, Sera, Kodi, taratibu za uendeshaji wa Vyama, uandishi wa Vitabu vya Hesabu, Bima, teknolojia na Viwanda vidogo ili kuimarisha utendaji na uchumi wa Wanachama na Jamii inayowazunguka vyama vya Ushirika.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Ushirika la Andrew Ntomola ambaye nae ametoa wito kwa Wanaushirika kutumia fursa ya Jukwaa hilo kujifunza kutokana na mada zinazowasilishwa kujiongezea maarifa, kupata huduma mbalimbali ikiwemo kujiunga na vyama vya Ushirika, huduma za mikopo nafuu na kubadilishana uzoefu. Jukwaa hilo linaendeshwa kwa Kauli mbiu ya “Ushirika unajenga kesho Bora kwa Wote”
Katika Jukwaa hilo jumla ya Vyama vya Ushirika wa kifedha na visivyo vya kifedha 32 vimeshiriki vikitokea katika Wilaya na maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dodoma pamoja na wadau wa Ushirika wakiwemo makampuni ya usambazaji wa Pembejeo, Wajasiriamali na Kampuni za Bima.
Mwisho