Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe, amewataka wadau wa zao la Tumbaku nchini kuwahamasisha wakulima wa zao hilo kulima mazao mengine kwenye maeneo yao badala ya kutegemea Tumbaku peke yake.

Waziri Bashe amesema hayo leo Februali 3, 2023 Jijini Dodoma kwenye semina ya sheria na sera mbalimbali za Sekta ya Tumbaku iliyoshirikisha kampuni za ununuzi wa zao hilo, wakulima na wadau wengine. Waziri Bashe amesema, kwa wakulima wa tumbaku kulima mazao mchanganyiko itawawezesha kunufaika zaidi kwani watakuwa wanapata mapato kutoka katika mazao tofauti tofauti.

“Wakulima hawa wa tumbaku ni lazima kuendelea kuelimishwa kuhusu umuhimu wa kulima mazao mchanganyiko kwa kuwa hatua hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kuwawezesha kunufaika zaidi na kilimo kwa kuwa watakuwa na wigo mpana wa mazao ya kuuza,” Waziri Bashe alisisitiza.

Ameongeza kuwa, iwapo ikitokea mkulima kapata tatizo lolote kwenye zao la Tumbaku anakuwa kwenye mazingira mazuri zaidi ya kupata kipato kwenye mazao  mengine kwasababu anakuwa hategemei zao moja. Amesema kuwa, Serikali itaendelea kupigania haki za wakulima nchini wakiwemo wakulima wa tumbaku ambapo amefafanua kuwa Wizara inazidi kujipanga katika kuhakikisha kuwa kilimo cha Tumbaku kinakuwa na tija kwa uchumi wa nchi na wakulima kwa ujumla.

Amesema kuwa katika kuhakikisha azma hiyo inatimia wizara imekuwa ikilinda maslahi yao hasa kwa kuwataka wafanyabiashara wanaotaka kuingiza Tumbaku kutoka nje ya nchi kuja kuwekeza kwenye zao hilo hapa nchini ili kuliongezea tija na kuliwezesha kuchangia kwenye pato la Taifa.

“Mimi kipaumbele changu imekuwa ni kuwasaidia wakulima na tena kuwawezesha wakulima kunufaika na kilimo na nitahakikisha kuwa wakulima wanazidi kunufaika," amesema. "Kumekuwa na mtazamo kuwa kilimo ni bidhaa ya jamii yani asiyelima amekuwa ni kama analima tutaubadili mtazamo huu,” Waziri Bashe alisisitiza.

“Katika kuhakikisha mkulima anazidi kunufaika wizara itafanya kila liwezekanalo kuhakikisha anapata faida na ifahamike kuwa tutaongeza uzalishaji ili kudhibiti mfumuko wa bei lakini siyo kwa kufunga mipaka,” amesema Mhe. Bashe.

MWISHO