Tume ya Maendeleo ya Ushirika  Tanzania, imewahamasisha wakulima wa mbogamboga na matunda kujiunga na vyama vya Ushirika ili kuleta tija katika shughuli za uzalishaji na kujikwamua kiuchumi.

Ushauri huo umetolewa na Ndimolwo Laizer kutoka  Tume ya Maendeleo Ushirika  wakati wa  utoaji wa elimu ya uhamasishaji kwa wakulima wa Mbogamboga wa vikundi vya  Nkoamala  na Jikomboe vilivyopo katika Kata ya Nkoandrua  katika Halmashuri ya Wilaya ya Meru,MKoani  Arusha.

Uhamasishaji huo umefanyika leo tarehe 14 Novemba 2022 ambapo Bw. Ndimolwo Laizer ametoa wito kwa wakulima hao kuunda Ushirika ili kilimo hicho kiweze kuleta tija zaidi na kujikwamua zaidi kiuchumi.

" Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania imeanzisha Programu  ya  uhamasishaji kwa wakulima wa mbogamboga kuunda Vyama vya Ushirika   katika Mikoa mitatu ya Tanzania Bara, ambayo ni Arusha, Njombe na Mbeya.

Katika Mkoa wa Arusha zoezi hili limeanza katika Halmashauri ya Meru na itaendelea katika Halmashairi za Arusha Vijijini na Karatu," alisema Laizer.

Aidha, Bw.Laizer alisema kuwa miongoni mwa  manufaa  ya Vyama vya Ushirika kwa  wakulima wa mboga mboga ni pamoja na kupanua mtaji  na kuimarisha nguvu ya kiuchumi kwa mkulima, kurahisisha  upatikanaji wa masoko ya mazao na bidhaa, pamoja na upatikanaji wa pembejeo na zana za kilimo kwa bei nafuu.

Nao  wakulima wa mbogamboga  wameishukuru Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa kukipa kipaumbele kilimo cha mbogamboga ambapo wameomba elimu hiyo kuwa endelevu ili kuwafikia wakulima wengi zaidi.

"Tunaishukuru Tume ya Maendeleo  kwa mpango mzuri waliotuletea wa kutuhamasisha kujiunga na vyama vya Ushirika; tunaamini mpango huu utakuwa mkombozi kwa maisha yetu," alisema Joseph Mbise mkulima wa mbogamboga toka kikundi cha Jikomboe.

Elimu hii ya kujiunga  na vyama vya ushirika pia imetolewa kwa  vikundi vya  Kwankiya na Warama katika Kata ya Maroroni.