Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa rai kwa Wakulima kujiunga na Vyama vya Ushirika ili kupata nguvu ya pamoja ya soko la mazao yao na kuwa na chanzo cha Mikopo na kuimarisha Maendeleo ya Ushirika hapa nchini.

"Kwa kutambua umuhimu wa Ushirika katika kuwaweka wakulima pamoja, Serikali inaendelea kuwahamasisha Wakulima, Wafugaji na Wavuvi kujiunga kwenye Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo yaani SACCOS vitakavyokuwa chanzo cha mikopo kwaajili ya kuendeleza shughuli zao na kuimarisha uwekezaji, katika Kilimo na Uvuvi lakini pia viwanda vya kusindika mazao ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi," amesema Makamu wa Rais..

Makamu wa Rais ametoa rai hiyo wakati akifungua Maadhimisho ya Maonesho ya Kwanza ya Kimataifa ya Wakulima alimaarufu Nanenene yanayofanyika kuanzia leo Agosti 01 hadi tarehe 8 Agost 2023 katika Viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya yenye kauli mbiu: Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa Mifumo endelevu ya Chakula.