Timu ya uhamasishaji kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) imekamilisha uhamasishaji wa uanzishaji wa Vyama vya Ushirika wa mazao ya bustani (horticulture) ambapo zoezi hilo lilifanyika kuanzia tarehe 24 Aprili hadi Mei 05, 2023 katika Halmashauri ya Wilaya za Moshi Vijijini, Moshi Manispaa na Hai. 

Ameeleza Afisa Ushirika kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika Ndimolwo Laizer kuwa uhamasishaji  huo umekamilika leo tarehe 05/05/ 2023  ambapo matarajio ya awali ni kuvifikia vikundi 18 vya wakulima wa mazao ya Bustani vyenye jumla ya wakulima 298 Baada ya zoezi kukamilika kwa halmashauri hizo jumla ya vikundi 48 vyenye Jumla ya wakulima 681 vimefikiwa na kupatiwa  elimu ya uanzishaji wa Vyama vya Ushirika vya Mazao ya Bustani mkoani humo.

Amesema hayo wakati wa uhitimishaji wa zoezi la utoaji elimu wa dhana ya Ushirika kwa lengo la uanzishwaji wa Vyama vya Ushirika leo tarehe 05/05/2023 katika Vijiji vya Mkalama kata ya Masama Rundugai na Kata ya Weruweru.


Amesema Ndimolwo Laizer Serikali imedhamiria kuwa kufikia 2030 wakulima wote Nchini wakiwemo wa MAZAO ya BUSTANI watakuwa wanazalisha kibiashara ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agenda 10/30 pamoja na faida mbalimbali zinazopatika kupitia Ushirika.

Kwa upande mwingine Afisa Ushirika Mwajuma Myombo  amesema kuwa Ushirika kwa Mazao ya Bustani utasaidia kurahisisha huduma zinazohitajika kwa wakulima ikiwemo huduma za ugani sambamba na kuongeza mapato kwa wakulima na Halmashauri husika.

Aidha, amesema kuwa kwa vikundi vilivyokubali kuanzisha Ushirika na ambavyo vimeanzisha Kamati anzilishi watashirikiana nao kuhakikisha mpaka tarehe zilizopangwa za kukutana tena nyaraka zote muhimu kwa ajili ya usajili wa Chama yatakuwa yameandaliwa.

Vyama vya Ushirika vya mazao ya Bustani 14 vinatarajiwa kuanzisha Mkoani Kilimanjaro na wakati wa utekelezaji wa zoezi la uhamasishaji jumla ya Vyama vya Ushirika sinzia 3 vya mazao ya mchanganyiko ikiwemo mazao ya Bustani vimefikiwa na kuhamasishwa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Masharti ya Chama, Sheria ya Vyama vya Ushirika na Miongozo mingine waliyojiwekea ili viweze kujibu hitaji la kuanzisha kwa Vyama hivyo.

Aidha,  zoezi litakalofuata ni la uandaaji na upitiaji wa nyaraka za usajili zitakazoandaliwa na Kamati anzilishi na kujadiliwa kupitia Mikutano Mikuu ya Kwanza ili Vyama hivyo tarajiwa viweze kusajiliwa.