Timu ya wataalam kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) kwa kushirikiana na wataalam wa halmashauri ya wilaya ya Hai imeendelea kufanya uhamasishaji wa uanzishwaji wa AMCOS za Mazao ya Bustani wilayani Hai.
Akizungumza na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Dionis Myinga, Afisa Ushirika kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), Ndimolwa Laizer , leo tarehe 02/05/2023 amesema azma ya serikali ni kuhakikisha kuwa wakulima wa Mazao ya Bustani wanazalisha kibiashara ikiwa ni utekelezaji wa Agenda 10/30: "Kilimo ni Biashara" ambapo kufikia mwaka 2030 wakulima wote nchini wakiwemo wa Mazao ya Bustani watakuwa wanazalisha kwa tija kwa mfumo jumuishi.
Kwa upande mwingine Mkurugenzi Myinga amesisitiza kuwa zoezi lifanyike kwa ufanisi ili wakulima wote wa mazao ya Bustani na mazao mengine wanahamasika kuanzisha Vyama vya Ushirika katika maeneo yao na yaendeshwe na kusimamiwa kwa mujibu wa Sheria na Miongozo iliyopo.
Wakulima hao wanaofanya shughuli zao za Kilimo cha mazao ya Bustani kupitia vikundi 15 katika Kata ya Kawaya (Kijiji cha Rundugai na Kawaya) na Kata ya Machame Narum wamepatiwa elimu ya dhana ya Ushirika na namna Vyama vya Ushirika vinavyowanufaisha wakulima Afisa Ushirika Ndimolwo Laizer wenye changamoto zinazofanana.
Wakati wa utoaji wa elimu, Laizer alisema kuwa wanachama wa Vyama vya Ushirika wanakuwa na fursa ya kupata elimu, mafunzo na taarifa ambapo Mafunzo hayo yanatolewa na wataalam kutegemeana na mahitaji ya kila Chama ambapo Chama itajitengea *10%* ya tengo la elimu kwenye ziada (faida) inayopatikana kwenye Chama kwa ajili ya Mafunzo kwa wanachama, Viongozi wa Bodi na watendaji wa Chama.