Mrajis wa Vyama vya Ushirikana Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege amevitaka Vyama vya Ushirika kushiriki Maonesho ya Kimataifa ya Biashara, makongamano na ziara za kibiashara kwa lengo la kujifunza, kufanya biashara na kuongeza wigo wa uzalishaji ili kukimbizana na fursa zilizopo na zinazojitokeza.
"Zama hizi wanaushirika wanatakiwa kutambua Ushirika ni biashara hivyo wachangamke katika kufanya Ushirika wa kibiashara na kuufanya Ushirika kuwa ni kimbilio la kila Mtanzania," amesema Dkt. Ndiege.
Ametoa kauli hiyo leo tarehe 09/07/2023 alipotembelea mabanda ya Ushirika katika Maonesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara maarufu SABASABA kwenye viwanja vya Mwl Julius Kambarage Nyerere.
Mrajis amesema maonesho hayo ni sehemu ya fursa kwa vyama vya ushirika na wanapaswa kutumia fursa hiyo ili waweze kuongeza fursa za kibiashara ndani na nje ya Vyama vyao.
Aidha, Dkt. Ndiege amevielekeza vyama vinavyofanya shughuli zaidi ya moja kuacha kuanziasha Vyama vingine isipokuwa waanze kuhuisha Masharti yao na kukifanya chama chao kuwa ni chama cha Ushirika wa Mazao mchanganyiko.
Naye Meneja wa Chama cha Ushirika cha DASICO LTD, Sijaona Mageta, amesema kupitia Sabasaba wamepata Kujitagaza na wanaendelea kupata oda kutoka kwa watu mbalimbali wanaohitaji huduma za thamani za majumbani na ofisini.