Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, ameagiza Vyama vya Ushirika kulipa fedha za mauzo ya Korosho kwa wakulima na kwa wakati.

Dkt. Ndiege mesema hataraji kuona wala kusikia malalamiko kutoka kwa wakulima wakidai katika AMCOS baada ya msimu wa mwaka huu kuisha.

Mrajis ametoa agizo hilo leo tarehe 16/11/2022 alipokuwa katika kikao kazi na Mameneja wa Vyama Vikuu na Wajumbe wa Bodi za Vyama Vikuu vya LINDI MWAMBAO, RUNALI, TANECU na MAMCU kilichofanyika mjini Mtwara.

Dkt. Ndiege alisema wajumbe wa Bodi wajibu wao ni kulinda maslahi ya wakulima, hivyo hatarajii kusikia manung’uniko ya aina yoyote kutoka kwa wakulima kuhusiana na malipo.

“Mpo katika nafasi hizo ili mseme na mtetee wakulima wetu, nyie msiwe katika mnaowakosesha haki zao  na AMCOS zenye hizo tabia mjitathimi kwasababu siwezi kuvumilia kuona wakulima wetu wanasononeka kwa ajili yenu,” amesema Dkt. Ndiege.
 
Aidha, aliwataka wajumbe wa bodi hizo kufanya kazi kwa kushirikiana na viongozi wa serikali na watumishi wa serikali ili kuweza kuwasaidia wakulima kupata stahiki zao na kutatua changamoto zao kwa uharaka zaidi.

“Mtambue Ushirika ni nguvu ya pamoja na ushirika ni mshikamano bila kuwa na mshikamano hamuwezi kufika kokote, mshikamane na muheshimu mamlaka iliyopo; una malalamiko fuateni utaratibu,” amesema Dkt. Ndiege.

Vile vile aliwakata kuhakikisha wanawasajili wakulima ambao si wanaushirika ila wanauza mazao yao kupitia AMCOS wapeni elimu wapunguzieni masharti ili wawe wanachama wenu.

Nao wajumbe wa Bodi za Vyama Vikuu wamemuomba  Mrajis kuangalia namna ya kubadili suala la muda wa kuongoza badala ya miaka 3 iwe miaka 5 ili wapate muda mrefu wa kufanya mambo ya maendeleo katika vyama vyao.

Pia waliomba kuwe na utaratibu wa kuchangia pembejeo kwa mkulima mwenyewe kulingana na uhitaji wake kwasababu wakulima wanapata
Pembejeo ambazo si uhalisia na uhitaji wao ili waweze kupata pembejeo ambazo zitaongeza tija katika uzalishaji wao.

Vile vile walisema elimu ya ushirika inaitajika sana mikoa ya Kusini ili waweze kuwa wanaongoza kwa kufuata taratibu, hivyo Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi waweze kufungua tawi la chuo hicho Mkoani Mtwara.