Katibu Tawala Mkoa wa Lindi Zuwena Omari ametoa wito kwa Vyama vya Ushirika Mkoani Lindi kuanzisha Viwanda vya kuchakata mazao ya wakulima ili kuongeza thamani pamoja na kuyatafutia masoko mazao hayo.
Amesema hayo Leo tarehe 4/06/2024 akiwa amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Lindi katika Jukwa la Ushirika wakati wa hitimisho la Jukwaa hilo liliofanyika kwa siku mbili Wilayani Ruangwa.
“Tukifanikiwa kuanzisha viwanda itasaidia wakulima kupata bei nzuri za mazao na kupandisha thamani ya mazao ya wakulima wetu,”amesema Katibu Tawala.
Awali, Katibu Tawala amefungua kituo cha malipo ya mazao cha Chama Kikuu cha Ushirika RUNALI na amesema ufunguzi wa kituo hiko maana yake wakulima watapata huduma ya malipo kwa haraka na malalamiko yatapungua kutokana na huduma kusogezwa.
Aidha, Katibu Tawala ameelekeza Vyama vyote vya Ushirika Mkoani humo kuhakikisha vinafunga mahesabu yao vizuri na nyaraka zitunzwe vizuri ili changamoto katika taarifa zenu za ukaguzi zisiwepo na zisiwe zinajirudia rudia kila zoezi la ukaguzi linapoanza.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa Maendeleo ya Ushirika mkoani Lindi,Odasi Mpunga amesema kupitia jukwaa hili elimu ya ushirika inaendelea kutolewa ili kuendelea kuwajengewa uelewa na uwezo zaidi wanaushirika na Wananchi kwa ujumla.
Naye Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Lindi, Cesilia Sostenesi, ameeleza kuwa Vyama vya Ushirika Mkoani humo vinajiendesha kwa kutumia mifumo ya TEHAMA na tayari Mfumo wa Kidigitali wa Usimamizi wa Vyama Vya Ushirika (MUVU) unatumika na Vyama vimesajiliwa katika mfumo na kwa mwaka wa fedha 2023/2024 vyama vya mazao vimepitishiwa bajeti zao katika mfumo wa MUVU.