Vyama vya Ushirika vya mazao vimetakiwa kuhakikisha vinatumia mizani ya kidigitali katika mauzo ya mazao ya Wakulima wakati wa msimu.

Hayo yameelezwa na Kaimu Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Consolata Kiluma, wakati akifungua kikao cha majadiliano kati ya TCDC, Vyama Vikuu vya Ushirika na Wawakilishi wa Benki ya CRDB kilichofanyika tarehe 20/01/2024 Jijini Dodoma.

Kikao hicho kililenga kupata ufafanuzi wa bidhaa ya  IMBEJU ambayo itawezesha upatikanaji wa mikopo ya riba nafuu hususan kwenye ununuzu wa mizani ya kidigitali.  

Naibu Mrajis Kiluma amesema Ushirika wa kianalojia umepitwa na wakati sasa tupo katika Ushirika wa kidigitali ndiyo maana suala la kutumia mizani hiyo ya kidigitali ni lazima kwa kila Chama.

“Kupitia mradi huu wa IMBEJU Vyama vitaweza kukopeshwa mizani hiyo kwa njia rahisi ila utaratibu wa  kuweka fedha kwa ajili ya kununua mizani ukaendelea kwaajili ya kulipa mizani hiyo iliyokopeshwa kupitia mradi huo na Benki ya CRDB,” amesema Naibu Mrajis.

Mkuu wa Biashara Changa kutoka CRDB  Benki, Fadhiri Bushagama, amesema Mradi  wa IMBEJU utamnufaisha mkulima mmoja mmoja na Chama kwa kupata mikopo ambayo haina riba na ambayo mkulima ambaye ni Mwanaushirika anaweza kukopa kuanzia Shilingi Millioni moja mpaka 10 na Mwanachama anaweza kulipa deni hilo kwa makubaliano ya kufuata ratiba za mauzo ya  mazao katika Vyama vyao.

Aidha, amewaomba Viongozi kuhakikisha wanasimamia suala  la urudishwaji wa mikopo baada ya kuanza makubalianao hayo ili na wengine waweze kuendelea kupata huduma na pia wasimamie suala la wanachama kupata mitaji katika Vyama vyao.

Naye Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Simiyu (SIMCU), Lazaro Walwa, amesema  mpango huo ni mzuri kwani utasaidia sana kwa wanachama kupata mitaji ila pia itarahisisha zoezi la upatikanaji wa mizani ya kidigitali.