Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika - Usimamizi na Udhibiti, Collins Nyakunga, amevitaka Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo (SACCOS) kutumia Vyombo vya Habari na Mitandao ya Kijamii kujitangaza.
Nyakunga amesema, vyama hivyo vinafanya mambo mengi mazuri ambayo yanapaswa kufahamika kwa jamii na kueleza ni vyema vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuhusika katika kuvitangaza.
Nyakunga ametoa kauli hiyo leo tarehe 14/03/2023 wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Nne cha Mameneja wa Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo kinachofanyika kwa siku nne Jijini Dodoma.
Kauli mbiu ya Mkutano huo ni “Meneja Wajibika, Timiza wajibu wako Ongeza thamani kwa Huduma Bora”. Kauli mbiu iliyolenga kuongeza ari ya watoa huduma kwa wateja.
Naibu Mrajis Nyakunga amesema Ushirika ni sehemu sahihi ambayo mtu yeyote anapokuwepo anakuwa na uhakika kuwa wapo mahala salama patakapowafanya kunyanyuka kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja au kikundi.
Vilevile Nyakunga amehimiza uanzishwaji Benki ya Taifa ya Ushirika na amesema Benki ya Ushirika ikianzishwa itafikisha mbali Ushirika hivyo ni wajibu wa wanaSACCOS kuendelea kununua Hisa ambazo zitafanikisha benki hiyo kupata mtaji wa kuendesha na kuifanya kuwa ni benki ya Ushirika.
Amesema Nyakunga zipo SACCOS zenye mitaji mikubwa ambayo tunafikiri waanze kukopesha UNION ambazo fedha zao ni za msimu, tutakaa vikao na kujadiliana hili na kufikia makubaliano, ili hata UNION ambazo wanapata fedha kwa msimu wanunue hisa katika bank hiyo.
“UNION zikikopeshwa na SACCOS tunatarajia baada ya misimu miwili wawe wamemaliza deni ili kuwezesha UNION zingine kukopeshwa.
"Tutakuwa makini sana katika kusimamia ulipaji wa deni hilo hivyo wakopeshwaji wanapaswa kutambua ukikopa lazima ulipe na na ulipe kwa wakati mliokubaliana,” Nyakunga alisisitiza.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji SCULLT (1992) Ltd, Hassan Mnyone ameeleza kuwa, kila Meneja anapaswa kuwa mbunifu katika kazi zake ili aweze kuendesha SACCOS yake na kuifanya izidi kukua na kuwa imara kila siku na kueleza siku ya jana ya Meneja haipaswi kufanana na ya leo.
Aidha, amesema ili kupata matokeo chanya katika vyama ni wajibu wa Meneja kufanya kazi kwa kujituma na kusimamia SACCOS kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni ziendele kuwa hai.
Vile vile amewaasa Mameneja hao kufanya kazi kwa maslahi ya wanachama na si kujiangalia wenyewe kwani Nguzo ya chama ni wanachama hivyo wajitahidi kupokea marekebisho na maoni yanayotoka kwa wanachama kwa Lengo la kujenga Vyama.