Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Dkt. Mussa Ali Mussa, ametoa wito kwa viongozi wa Vyama vya Ushirika kufanya shughuli zao kwa lengo la kuwainua kiuchumi wanachama na kuacha kujinufaisha wenyewe.

Dkt. Mussa amesema ni wajibu wa Viongozi kufanya kazi kwa lengo la kuinua uchumi wa wanachama wao na wa wakulima kwa ujumla, na kuacha kujinufaisha wao wenyewe na kusahau wajibu wa kuhudumia na kusaidia wanachama na wakulima.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro ametoa kauli hiyo leo tarehe 07/12/2022 alipokuwa akifungua Mafunzo ya Mfumo wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (MUVU) Mjini Morogoro uliowakutanisha Warajis Wasaidizi, Maafisa Ushirika wa Mkoa wa Pwani, Morogoro, Mameneja na Wenyeviti  wa Vyama Vikuu vya Ushirika.

Dkt. Mussa amesema kuna vyama vimekuwa vinamiliki mali na mali hizo zimekuwa zinanakiliwa kwenye makaratasi ambayo yanaweza kupotea, kuchanika; lakini  Mfumo wa MUVU utasaidia vyama kuhifadhi taarifa zao kwenye mfumo ambao hautokuja kupoteza taarifa hizo.

“Kuna viongozi wajanja wajanja wanatumia nafasi zao vibaya wanajimilikisha mali za chama wanaibia vyama ila kwa mfumo huu mambo ya kujimilikisha au kuwaibia wanachama itakuwa imekwisha kabisa. Na hakikisheni kila chama kinakuwa na vifaa vya kielekroniki ili iwe rahisi kufanya kazi,” amesema Dkt. Mussa.

Dkt. Mussa amesema kuwa matumizi ya TEHAMA kwa dunia ya sasa ni lazima, hivyo ni wajibu wa washiriki wa mafunzo haya kuzingatia wanachofundishwa ili wakirudi katika maeneo yao ili iwe rahisi kuendelea kufanyia kazi Mfumo wa MUVU.
 
Naye Mwenyekiti wa Mafunzo hayo, Mhasibu Mkuu Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Valency Karunde, amesema lengo la mafunzo hayo ni kurahisha utendaji kazi wa vyama na Usimamizi wa Tume kwa vyama hivyo.

Amesema hadi sasa mafunzo haya ya awamu ya kwanza yametolewa kwa Warajis Wasaidizi, Maafisa Ushirika, Mameneja  na Wenyeviti wa Vyama Vikuu wa Mikoa 17 na awamu ya pili watapatiwa Makatibu au Mameneja wa vyama vya Msingi katika Mikoa yote.

 Karunde amesema TCDC imedhamiria kuhakikisha kila Mrajisi na Afisa Ushirika anakuwa na vifaa kama Kompyuta. Tume imenunua Kompyuta 103 na kuzigawa kwa Warajis Wasaidizi wa Vyama vya Ushirika wa mikoa na Maafisa Ushirika walioko Mkoani na Wilayani.