Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameunga mkono mageuzi yanayofanyika katika Vyama vya Ushirika nchini ili kulinda maslahi ya Wanaushirika na kurudisha hadhi ya Ushirika.
Akizungumza na Wanaushirika na Maafisa Ugani katika mkutano uliofanyika katika Ikulu ya Chamwino, Jijini Dodoma leo, Agosti 10, 2024, Rais Samia amesema Vyama vya Ushirika ndiyo chombo madhubuti kinacholeta Maendeleo kwa watu wengi na kutondoa matabaka.
"Wanaushirika mmeanza kufanya mabadiliko muhimu yanayohitajika, ninawapongeza na endeleeni kusimamia vema maslahi mapana ya Wanaushirika," amesema Mhe. Rais.
Aidha, Mhe.Rais amewapongeza Wanaushirika kwa kuamua kuachangishana na kuanzisha Benki ya Taifa ya Ushirika nchini, ambayo itakuwa ngao yao katika upatikanaji wa fedha za mitaji kwa Vyama na Wanaushirika.
"Serikali inawapongeza kwa uamuzi huu muhimu wa kuanzisha Benki yenu Wanaushirika; na Serikali itawaongezea Shilingi Bilioni tano (5) katika mtaji wa kuanzisha Benki hii muhimu kwa Wanaushirika na Wananchi kwa ujumla," amesema Mhe. Rais.
Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewapongeza Maafisa Ugani na watumishi wa Wizara ya Kilimo kwa kufanikisha nchi kujitosheleza kwa chakula na kuwa na ziada.