Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson, amewataka Viongozi wa Vyama vya Ushirika Nchini kutekeleza maeneo 7 muhimu ya kuzingatia katika uendeshaji wa Vyama ili kuleta mabadiliko katika Sekta ya Ushirika.

Mrajis ameyataja maeneo hayo saba leo tarehe 11 Septemba 2023 alipokuwa akiwasilisha Taarifa ya  Hali ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania Bara katika kikao cha Warajis Wasaidizi na Watendaji wa Vyama kilichofanyika Jijini Dodoma.

"Tume na wadau wa Ushirika tumekubaliana kwamba Maeneo haya saba ndiyo yawe mwongozo na mwelekeo wa Maendeleo ya Ushirika," amesema Dkt Ndiege.

Akiyataja maeneo hayo saba kuwa  ni: Uwekezaji katika mifumo ya kisasa ya kidigitali; uanzishaji wa Benki ya Taifa ya  Ushirika; kuhamasisha Mfumo wa Ushirika kujiendesha kibiashara; Usimamizi wa Vyama vya Ushirika; kuhamasisha Ushirika kwenye Sekta mbalimbali na makundi maalum; kushirikiana na wadau mbalimbali kutatua changamoto za Ushirika; na kuimarisha uwekezaji wa Mali za Ushirika katika uzalishaji.

"Lengo la kikao hiki ni kupata komitment ya kila mkoa kwenye maeneo haya,wao wamejipangaje ndipo tutauweka Ushirika mahali pake" ameongeza  Mrajis.

Aidha, katika kikao hicho Dkt.Ndiege amewapongeza Watendaji mbalimbali wa Vyama vya Ushirika, wakiwemo Maneneja na Wenyeviti wa Vyama kwa kufanya Vizuri katika kuleta maendeleo na kuujenga Ushirika mpya.

"Hongereni sana, mnafanya vizuri, kazi mnayofanya ni nzuri na inaonekana," amesema Dkt.Ndiege.