Kaimu Naibu Mrajis (Uratibu  na Uhamasishaji) wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania(TCDC), Consolata  Kiluma, amewataka Viongozi na Watendaji wa Vyama vya Ushirika mkoani Shinyanga kuondokana na Hati Chafu ili kuwa na Ushirika  wenye tija.

Wito huo umetolewa leo terehe 06/03/2023 katika Jukwaa la Maendeleo  ya Ushirika   mkoani Shinyanga lenye lengo la kujadili changamoto, mafanikio na maazimio ya Ushirika  kwa ujumla.

"Nitoe wito kwa watendaji wa Ushirika kuondokana na Hati Chafu, tujadiliane na tusaidiane kama Wanaushirika, namna gani tutafanya kuweza kuepukana na changamoto zinazoweza kujitokeza kuhusiana na Hati Chafu," amesema Kiluma.

Aidha, Kaimu Naibu Mrajis  amewataka wanaushirika  kuendelea kuchangia Benki ya Ushirika  ya Kilimanjaro (KCBL) ili kuweza kukamilisha uanzishwaji wa Benki ya Taifa ya Ushirika ambayo ni mkombozi mkubwa kwa Wanaushirika kwa ujumla.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa amewataka Viongozi wa Vyama Vya Ushirika  kuwa mfano kwa Vyama wanavyoviongoza.
 
"Unapopewa dhamana ya Uongozi unatakiwa kuwa mfano kwa wakulima, kiongozi unatakiwa kuwa na Shamba la mfano ili kuweza kusimamia vizuri za wakulima. Huwezi kujadili Changamoto  za Wakulima wakati huna shamba, usipofanya vigumu kujua changamoto wanazozipitia Wakulima," amesema Mlolwa.

Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani, ambaye pia ni mwanaushirika amesema kuwa ili kuweza kuwa na Hati Safi yawapasa viongozi kusimamia watendaji wa Vyama vya  Ushirika kuandika vitabu, kufunga Hesabu ili kusaidia kuwa na namna bora ya matumizi bora ya Fedha.

"Ushirika kwa Sasa unafanya vizuri,Viongozi wasaidieni Vijana kuandika vitabu na kufunga mahesabu ili kuondokana na Hati Chafu," amesema Mhe. Cherehani.

Katika katika jukwaa hilo Ofisi ya Mrajis  mkoa wa Shinyanga imetoa Tuzo mbalimbali kwa Vyama vya Ushirika vilivyofanya vizuri katika utendaji kazi kwa kuwa wabunifu, uwezo na utoaji wa huduma bora kwa wakulima.Vyama vilivyopata tuzo hizo ni UDIDA SACCOS, IPANDIKILO SACCOS, Chama Kikuu cha Ushirika - KACU, NGOKOLO AMCOS, Shinyanga Municipal SACCOS na Biashara SACCOS.

Akiongea mara baada ya utowaji wa tuzo hizo, Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Shinyanga, Hilda Boniphace, amevitaka Vyama kuendelea kufanya vizuri kwa kufuata taratibu na Sheria za Vyama vya Ushirika.