Wakurugenzi wakuu wa Bodi za Mazao na Taasisi za utafiti wa Kilimo wamepatiwa maelezo ya namna Mfumo wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (MUVU) unavyofanya kazi katika Vyama vya Ushirika.

Maelezo hayo yametolewa na Mkuu wa kitengo cha TEHAMA Bwana Hermis Rulagirwa leo  tarehe 11/11/2022 wakati wa kikao cha Viongozi Taasisi za Utafiti wa Kilimo na Bodi za Mazao kuhusu namna ya kudhibiti ongezeko la Magonjwa na Wadudu waharibifu wa Mazao kilichofanyika katika ukumbi wa Posta, Morogoro Mjini.

Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, ameeleza kuwa maoni na ushauri uliotolewa na Viongozi wa Bodi za Mazao na Taasisi za Utafiti utafanyiwa kazi na maboresho yatafanyika kwa uharaka ili mfumo uwe rafiki katika utendaji kazi.

Dkt. Ndiege amesema kama vyama vyote vya Ushirika vitazingatia na kuanza kutumia Mfumo huu wa kidigitali basi mkulima ataweza kuhudumiwa kwa uharaka na urahisi.

“Suala la Vyama vya Ushirika kuleta makisio ya bajeti na matumizi yao kwenye ofisi za Tume Dodoma litakuwa limeisha kwasababu watakuwa wanatuma kupitia mfumo huo na kupata majibu kutoka kwa Mrajis kwanjia hiyo hiyo ya mfumo,”  amesema Dkt. Ndiege

Aidha, Mrajis  amewaomba Viongozi hao waendelee kuvihamasisha Vyama vya Ushirika kuhama katika mfumo wa makaratasi na kuhamia kwenye Mfumo wa kidigitali.

Viongozi wa Bodi za Mazao  wameiomba TCDC kuendelea kutoa mafunzo ya mfumo huo katika vyama vya Ushirika  na pia kuhakikisha kila kiongozi anajua namna ya kutumia na kuumiliki Mfumo wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika.