"USHIRIKA NINA UHAKIKA UKO SALAMA" - WAZIRI MKUU

 

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, ameipongeza Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) kwa jitihada zake za kuhakikisha Ushirika unastawi na kuwa sehemu sahihi na salama ya uwekezaji wa mali za wanaushirika na wadau wengine ikiwa ni pamoja na kuinua uchumi wa mwanachama na Taifa kwa ujumla.

“Naipongeza  Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa jitihada zake za kuhakikisha Ushirika unastawi na kuwa sehemu sahihi na salama ya uwekezaji wa mali za wanaushirika na wadau wengine ikiwa ni pamoja na kuinua uchumi wa mwanachama mmoja mmoja na pato la taifa Nina uhakika Ushirika uko salama,” amesema Waziri Mkuu.

Ametoa pongezi hizo jana tarehe 04/08/2022, alipofanya ziara ya kutembelea 'Kijiji cha Ushirika' kwenye Maonesho na Maadhimisho ya NANENANE Kitaifa yanayofanyika kwenye viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya.

Katika msafara wake, Mhe. Waziri Mkuu aliambatana na viongozi mbalimbali wa Serikali, akiwemo Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Akson na Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Anthony Mavunde.

Aidha, Mhe. Majaliwa ameiagiza TCDC kuendelea kusimamia Ushirika kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo ya Ushirika na kusisitiza wadau washiriki kuhamasisha Vyama vya Ushirika, wanachama wa Vyama vya Ushirika na wadau wengine kuwekeza kupitia benki ya KCBL kwa kununua hisa ili kufanikisha adhma ya Serikali ya kuanzisha benki ya Taifa ya Ushirika.

Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Ushirika Tanzania, Dkt. Benson Ndege, aliwasilisha taarifa fupi ya Maendeleo ya Sekta ya Ushirika kwa Mgeni Rasmi ikiwa ni pamoja na taasisi na wadau waliopo ndani ya Kijiji cha Ushirika kwenye Maonesho na Maadhimisho ya NANENANE.