Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, amesema Tume itaendelea kusimamia Vyama vya Ushirika kwa kutumia njia za kisasa za Kidigitali ambazo zinaongeza tija, ufanisi, uwazi na uwajibikaji na utakaosaidia kuimarisha na kuendeleza Ushirika nchini. 

Akiongea wakati wa kikao na Waandishi wa Habari kwenye Ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO Agosti 11, 2023 Jijini Dodoma amesema hadi kufikia Juni 2023, vyama vya Ushirika 5,424 kati 7,300 vimesajiliwa katika Mfumo wa kidigitali wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (MUVU).

“Mfumo wa MUVU unasaidia kupunguza gharama za uendeshaji, kuwa na uhakika wa kupata takwimu na kuimarisha utendaji/uendeshaji wa Vyama,” amesema Mrajis 

Ameongeza kuwa kupitia Mfumo wa MUVU, Vyama vya Ushirika vinaweza kuwasilisha taarifa za Ukaguzi, mapato na matumizi ya Vyama, taarifa ambazo zinawasilishwa kwa urahisi na kuwafikia Maafisa Ushirika wa Wilaya, Warajis wasaidizi wa Mikoa na Ofisi ya Mrajis Taifa kwa lengo la kusimamia utendaji wa Vyama pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji.

Aidha, Tume katika jitihada za kuimarisha Ushirika Mrajis amesema kuwa mwaka 2022/2023 imeendelea kuhamasisha uanzishwaji wa Benki ya Taifa ya Ushirika (KCBL) ili kutatua changamoto ya mtaji katika uendeshaji wa vyama vya ushirika nchini. Mikakati mbalimbali inatekelezwa itakayowezesha upatikanaji wa mtaji wa Shilingi Bilioni 15 unaotakiwa kisheria ili iweze kusajiliwa kama Benki ya Taifa ya Ushirika.  

Pamoja na mambo mengine Mrajis amesema vipaumbele vya Tume ni pamoja na  kuhamasisha mfumo wa Ushirika kujiendesha kibiashara, kuhamasisha Ushirika kwenye sekta mbalimbali na makundi maalum ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wananufaika na mfumo wa Ushirika.

Aidha, Mrajis amesema TCDC imedhamiria kuimarisha uwekezaji wa mali za Ushirika katika uzalishaji; na kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutatua changamoto zilizopo kwenye Ushirika.