Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Emil Kasagala, leo tarehe 26 Oktoba 2022, amefungua  Mafunzo ya Mfumo wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (MUVU)  kwa upande wa Kanda ya Ziwa   yanayofanyika ukumbi wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Jijini Mwanza. Mafunzo  yatafanyika kwa siku tatu kuanzia leo hadi 28/10/2022.

Bw. Kasagala amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi ya uanzishwaji na uendelezaji wa Vyama vya Ushirika ili kuhakikisha Vyama vinakidhi matakwa ya wanachama na kuchangia maendeleo ya Taifa na kumaliza  changamoto mbalimbali katika  uendeshaji na usimamizi wa Vyama vya Ushirika nchini.

Alieleza kuwa kumekuwa na Ugumu wa kuhuisha Daftari la usajili wa Vyama na wanachama na  utendaji usioridhisha kutokana na ukosefu au upungufu wa uwazi katika uendeshaji na usimamizi wa rasilimali za vyama hivyo kuwepo na utendaji kazi usioridhisha, unaotokana na ukosefu wa uaminifu na kutokuwepo na uwajibikaji ndani ya Vyama.

Bw. Kasagala amesema kuwa kumekuwa na ukosefu wa taarifa sahihi na kwa wakati, kutokana na mifumo duni ya mawasiliano pamoja na uhifadhi duni wa nyaraka na kumbukumbu za Vyama inayosababisha   baadhi ya Vyama kupata Hati Chafu za Ukaguzi.  

 "Mnaopata mafunzo haya mjitahidi kuyafanyia kazi ili kuondoa hali zilizokuwepo zamani za kutokuwepo na mfumo thabiti wa ufuatiliaji wa ukaguzi, usimamizi wa vyama pamoja na mrejesho kwa wakati hasa kwa wakulima juu ya mauzo, masoko, malipo, uwekezaji, faida, ukosefu wa taarifa sahihi za mnyororo wa masoko kwa wakulima; na kukosekana kwa usahihi wa taarifa za mikataba," amesema Kasagala.

Aidha, Bw   Kasagala amewataka Wenyeviti wa Vyama katika Mafunzo haya kuzingatia elimu wanayoipata ya kutumia Mfumo kwa ajili ya faida ya vyama vyao kwani wao ndiyo watakaoenda kuwasimamia na kuwaongoza wanachama wengine wa ushirika.

"Hivyo ni muhimu na lazima mhakikishe  mnaelekeza nguvu na uelewa wenu katika mafunzo haya, ili mkitoka hapa mwendelee na utekelezaji. Ikumbukwe wewe Mtandaji (Meneja au Karani) ndiyo nguzo ya Mfumo huu na tumechoka kuona mnapata Hati Chafu mara kwa mara; nina imani kupitia mfumo huu suala la Hati Chafu limefika mwisho wake," amesema Kasagala.

MWISHO