Mkuu wa Wilaya ya Chemba Mhe. Halima Okash amewataka watendaji kusimamia ipasavyo miradi ya Maendeleo katika Wilaya ya Chemba ili kuendana na kasi ya utendaji wa Serikali ya Awamu ya Sita kwa lengo la kuwaletea maendeleo Wananchi.
Ameyasema hayo akifungua Mkutano wa Baraza la Waheshimiwa Madiwani la Robo ya Kwanza ya mwaka wa Fedha 2024/25 uliombatana na mafunzo ya Ushirika kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) kwa Madiwani na Viongozi wa Halmashauri ya Chemba Novemba 1, 2024 Jijini Dodoma.
Aidha, katika Mkutano huo Naibu Mrajis Consolata Kiluma akitoa mafunzo ya Ushirika amesema Vyama vya Ushirika ni nyenzo muhimu inayotumika katika ukusanyaji wa mazao, unaochangia katika kuongeza mapato kwa Serikali na tija ya bei yenye ushindani kwa Wakulima kutokana na nguvu ya soko katika uuzaji wa mazao.
Pamoja na mambo mengine Naibu Mrajis amebainisha taratibu za uanzishaji wa Vyama vya Ushirika, Sifa za uanachama, Sheria na taratibu za kufuata katika usajili wa Vyama pamoja na umuhimu wa matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi ya Ghala kupitia Ushirika katika kuongeza tija na mapato kwa Wakulima.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani Halmashauri ya Chemba Mhe. Said Sambala ametoa Rai elimu ya Ushirika iendelee kutolewa katika Halmashauri hiyo hadi kwenye Tarafa mbalimbali za Wilaya ili Wananchi waweze kuwa na uelewa mpana wa Ushirika pamoja na Mfumo wa Stakabadhi ya Ghala.
Mkutano huo wa Baraza la Madiwani umehudhuriwa Viongozi mbalimbali wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba akiwemo Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Kunti Majala, Wakuu wa Idara, Sehemu wa Halmashauri hiyo.