Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) na Kampuni ya Tigo imesaini Randama ya Makubaliano (MoU) kwa ajili ya kutoa huduma ya malipo kwa wakulima kwa Tigo Pesa wanaouza mazao kupitia Vyama vya Ushirika.
Makubaliano hayo yametiwa saini leo tarehe 30/01/2024 Jijini Dodoma ambapo Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa TCDC, Dkt. Benson Ndiege, amesema kuwa Tume ikiwa Msimamizi wa vyama vya ushirika, inataka kuona kila Mwanaushirika na Mkulima anapata fedha yake kwa urahisi na kwa wakati anapouza mazao yake kupitia Ushirika na Stakabadhi za Ghala.
Dkt. Ndiege ameeleza kuwa uwepo wa makubaliano hayo utawezesha Kampuni ya Tigo kutoa huduma ya Malipo kwa wakulima sambamba na kushirikiana na Tume kutekeleza mipango ya kiserikali ambayo itawezesha wakulima na wananchi kunufaika na shughuli zao kupitia Ushirika.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Tigo, Angelica Peshawar, amesema Randama iliyosainiwa ni muendelezo wa Randama uliyoisha mwaka jana 2023 ambayo Utekelezaji wake ulifanya vizuri kutokana na usimamizi wa pande zote mbili na ndiyo umepelekea kusainiwa Randama mpya.
“Niendele kuishukuru TCDC kwa kuendelea kutuamini na kuendelea kufanya kazi pamoja na sisi na tunaahidi kuja na mpango mpya utakaomsaidia mkulima katika kuwezesha kukua kiuchumi zaidi,” amesema Peshawar.