Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) na Taasisi ya Hanns R. Neumann Stiftung (HRNS) zimesaini Randama ya makubaliano ya kuviimarisha Vyama vya Ushirika katika mikoa ya Mbeya, Songwe na Ruvuma.

Makubaliano hayo yamefanyika leo tarehe 02/11/2022 katika Ofisi za Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Jijini Dodoma.

Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, Dkt. Benson Ndiege ametoa wito kwa Taasisi ya HRNS kuongeza wigo katika Mikoa mingine ili kuweza kuvifikia vyama vingine vya ushirika nchini.

“Kipindi cha miaka mitatu mmefanya kazi na vyama vya ushirika 15 tu nafikiri ni wakati wa kujitanua kwenda maeneo mengine kwasababu Wanaushirika wapo kila maeneo na wanahitaji kupata mafunzo mnayotoa,” amesema Dkt. Ndiege.

Aidha, Dkt. Ndiege amewapongeza HRNS kujikita zaidi kwa Vijana na Wanawake katika ushirika, kwani Tume ina malengo ya kuhakikisha kila Vijana na Wanawake wanajiunga na ushirika kwa lengo la kuboresha maisha yao.

Naye  Meneja Mkuu wa Shirika la HRNS Tanzania, Morgan Mkonyi ameishukuru  Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa namna inavyowapatia ushirikiano katika utendaji kazi wao ambao unarahisisha  utendaji kazi wao.

Bw. Mkonyi amesema Mkataba uliosainiwa ni mwendelezo wa mkataba wa mwanzo wa miaka mitatu ulioanza tarehe 11/7/2019 na kuisha 11/7/2022 uliokuwa unalenga kutoa mafunzo kwenye vyama vya ushirika vya Kahawa, kuunganisha vyama na watoa huduma mbalimbali na maeneo mengine ya kimkakati na mkataba huu mpya utagusa maeneo ya Ruvuma na Mbeya na Songwe.