Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, amemhakikishia Mkurugenzi wa kiwanda cha mbolea cha INTRACOM kuwa mikataba itakayoingiwa na Vyama Vya Ushirika na Kiwanda hicho itasimamiwa ipasavyo na TCDC.

“Nikutoe hofu na nikuhakikishe tutafanya kazi nzuri kwasababu hakutokuwa na Risk ya kupoteza chochote katika makubaliano yetu kwasababu tunaingia mkataba na Chama na si mtu mmoja mmoja,” amesema Dkt. Ndiege.

Ametoa kauli  hiyo leo tarehe 30 Novemba, 2023 wakati wa kikao na Viogozi wa Vyama Ushirika vya MBIFACU LTD, CHUTCU LTD, TANECU LTD, KACU LTD, SORECU LTD, CORECU LTD, KDCU LTD, WETCU LTD, WAMACU LTD, LINDI MWAMBAO, RUNALI, NGARA FARMES, IFCU LTD, UFIPA CU LTD, TAMCU LTD, TANCCOOPS LTD na TFC kiluchofanyika katika Kiwanda cha Mbolea cha  INTRACOM FERTILIZER LIMITED.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Mbolea   INTRACOM FERTILIZER LIMITED, Nduwimana Nazaire, amevikaribisha Vyama Vya Ushirika ofisini kwake ili kujadili namna ya kuanza kufanya kazi na Vyama hivyo kwa  kuwa Wakala wa mbolea ya Fomi na kuisambaza kwa wakulima wanaowahudumia.

Nazaire amesema hakuna kitakachoshindikana katika makubaliano yatakayofikiwa kwa lengo la kufanya biashara ambayo ni endelevu na kueleza  amefurahishwa na ugeni huo kiwandani hapo.

Naye Makamu  Mwenyekiti wa TANCCOOPS LTD, Zainabu Maheme, amesema anaushukuru uongozi wa TCDC kwa kuwatafutia fursa hiyo ambayo itawafanya waweze kuwahudumia vizuri wanachama wao katika suala la mbolea na kuomba INTRACOM kuwaamini ili waweze kufanya biashara.