Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, leo tarehe 22 Machi, 2023 ameshiriki Mkutano wa Fursa za Kibiashara na Masoko nchini Sudani ya Kusini ambapo amewahakikishia Wafanyabiashara wa nchi hiyo upatikanaji kwa wingi wa mazao bora ya kilimo kutoka Tanzania kupitia Vyama vya Ushirika na Mfumo wa Stakabadhi za Ghala.

Mkutano huo umeandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini Sudani ya Kusini, kwa lengo la kujadili na kuunganisha fursa za biashara na masoko ya mazao baina ya nchi hizi mbili, na utafanyika kwa siku mbili kuanzia leo tarehe 22 - 23 Machi, 2023.​

Katika mkutano huo, Mrajis amepata fursa ya kuwasilisha na kueleza fursa mbalimbali zinazopatikana kwenye Sekta ya Kilimo kupitia Vyama vya Ushirika. Baadhi ya maeneo yaliyoelezwa ni pamoja na uwepo wa fursa za masoko ya mazao na bidhaa zinazozalishwa na kuuzwa kupitia Vyama vya Ushirika, upatikanaji wa pembejeo za kilimo kupitia Vyama vya Ushirika, pamoja na uwekezaji katika Vyama vya Ushirika.

Aidha, Mwakilishi wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala, Erick Temu, wameeleza namna Mfumo wa Stakabadhi za Ghala unavyofanya kazi na kutoa fursa kwa wafanyabiashara kupata mazao yenye ubora kupitia Vyama vya Ushirika.

Mkutano huo unafanyika Mjini Juba na unahudhuriwa na Wakuu wa Taasisi za Serikali pamoja na Sekta Binafsi kutoka Tanzania.

Taasisi za Serikali zinazoshiriki ni pamoja na Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Hospitali ya Muhimbili, Shirika la Bima la Taifa (NIC), Shirika la Posta Tanzania (TPC), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Tume ya Ushindani Tanzania, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Shirika la Ndege Tanzania (ATC), Mamlaka ya Usimamizi wa Petroli Tanzania (PURA), VETA na Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA). Kwa upande wa Sekta Binafsi, makampuni yanaoshiriki mkutano huo ni Kampuni ya Tobage, Junaco na Kusa Investment na SUMA JKT.