Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika imetoa mafunzo kwa Maafisa Ushirika, Maafisa  TEHAMA, Mameneja na Warajis Wasaidizi wa Vyama vya Ushirika wa mikoa ya Tabora, Kigoma, Katavi na Singida.

Akifungua mafunzo ya Mfumo wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (MUVU) mjini Tabora leo tarehe 23/11/2022, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt. John Mboya ameipongeza Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania kwa kuanzisha Mfumo huo na kutoa Mafunzo ya matumizi yake kwa walengwa.

"Tunaishukuru Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika kutuletea mafunzo haya ya Mfumo wa kiteknolojia wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika ambapo mfumo huu utasaidia kurahisisha Vyama vya Ushirika kufanya shughuli zote katika mfumo, hivyo kurahisisha utendaji kazi kwa maafisa Ushirika na kwa Wanaushirika walioko kwenye vyama vya Ushirika," alisema Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora Dkt. Mboya.

Aidha, Dkt. Mboya amesema  kuwa ili Taifa letu liwe shindani lazima tuwe katika Mfumo wa kiteknolojia ambapo mfumo huu ni kiungo muhimu katika kuleta mapinduzi katika kilimo na Uchumi kwa ujumla.

Naye Mwakilishi wa Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, ambaye ni Mhasibu Mkuu Bwana Valency Karunde amesema Mfumo wa MUVU utasaidia kurahisisha Vyama vya Ushirika kufanya shughuli zote katika mfumo hivyo kurahisisha utendaji wa kazi katika Vyama vyote vya Ushirika hapa nchini.

Akiongea kwa niaba ya washiriki wa Mafunzo hayo, Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Katavi, Peter Nyakunga, amesema Mafunzo na matumizi ya MUVU yatawarahisishia  kama watendaji wa vyama vya Ushirika kupata taarifa mbalimbali katika mfumo, utunzaji wa kumbukumbu na vile vile kuwasaidia wakulima kupata taarifa sahihi na kwa wakati.

"Tunaomba Mafunzo haya yawe endelevu kwa Maafisa Ushirika kote nchini ili kuwajengea uwezo wa kutumia Teknolojia ya kisasa ambayo ni chachu kwa Maendeleo ya Sekta ya Kilimo na Taifa kwa ujumla," alisema Nyakunga.