VYAMA VYA USHIRIKA WA AKIBA NA MIKOPO (SACCOS) VYATAKIWA KUFUNGA HESABU KWA MWAKA WA FEDHA UNAOISHIA DESEMBA 31, 2020

 

Mwaka wa Fedha wa Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) unaanzia Mwezi Januari na kuisha Mwezi Desemba kila mwaka. Mara baada ya kupita kwa muda huo, Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, amezitaka SACCOS zote kuhakikisha zinafunga Hesabu zake za Mwaka husika kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 55(2) cha Sheria ya Vyama vya Ushirika Na.6 ya Mwaka 2013 na kanuni ya 55 ya Kanuni za Vyama vya Ushirika za Mwaka 2015 na kutakiwa kuziwasilisha kwa Mkaguzi wa Nje (Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika - COASCO).

 

Katika kutekeleza matakwa haya ya Sheria na Kanuni, Mrajis amewaelekeza Viongozi wa SACCOS nchini kuhakikisha wanafunga Hesabu za Mwaka 2020 mapema na kuziwasilisha kwa Wakaguzi wa Nje ndani ya Mwezi wa Januari 2021, ili hesabu hizo ziweze kukaguliwa na kurudishwa kwao mapema.

 

Viongozi wa SACCOS wanapaswa kujibu hoja zote zilizotolewa na zitakazotolewa na Wakaguzi ili kuondokana na uwepo wa Hati Zisizoridhisha pamoja na Hati Chafu. Chama kitakachoshindwa kujibu hoja husika na kupata Hati Chafu, Viongozi na Watendaji wake watapaswa kuwajibika kwa kuzingatia matakwa ya Kifungu cha 55(13) cha Sheria ya Vyama vya Ushirika, kanuni ya 85(g) ya Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha (SACCOS) za Mwaka 2019.  

 

Ofisi ya Mrajis katika ngazi ya Taifa na katika mikoa yote itafuatilia utekelezaji wa maelekezo haya kwa karibu na kuchukua hatua stahiki kwa wote watakaobainika kwenda kinyume na maelekezo haya na kushindwa kutekeleza matakwa ya Sheria na Kanuni zake kama zinavyoelekeza.

 

Aidha, Mrajis amewakumbusha na kuwahimiza viongozi wa SACCOS nchini kuhakikisha wanaomba Leseni kwa wakati ili kuepuka usumbufu na adhabu zinazoweza kutolewa kwao iwapo watashindwa kuomba na kupata leseni kwa wakati katika kipindi cha mpito kilichotolewa na Serilikali. Hesabu zilizokaguliwa na Mkaguzi wa Nje zinatakiwa kutumika katika zoezi la kuomba Leseni kwa SACCOS, ambazo hazijaomba leseni hadi kufikia tarehe ya Taarifa hii.

 

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC)