Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mheshimiwa Dkt Yahaya Nawanda , ametoa Rai kwa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Simiyu (SIMCU - 2018) Ltd kufufua Viwanda vyao na kuanza kufanya kazi ili kuimarisha Mnyororo wa thamani wa zao la Pamba.
Dkt Nawanda amesema SIMCU (2018) Ltd wanatakiwa kukifanya kilimo cha Pamba kuwa chenye tija na thamani kwa wakulima na jamii kwa ujumla kwani Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameweza kuongeza bei ya pamba kutoka Shilingi 1,200 msimu 2021/22 hadi Shilingi 2,050 msimu huu 2022/23.
Dkt. Nawanda ametoa rai hiyo alipokua akihutubia wakati wa Mkutano Mkuu wa Sita wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Simiyu SIMCU (2018) Ltd akiwa ni Mgeni Rasmi katika mkutano huo uliofanyika tarehe 17/ 03/ 2023 Mkoani Simiyu.
Mgeni Rasmi amesema Mkoa wa Simiyu ni mkoa pekee unaolima Pamba Hai “Organic Cotton” na kuwataka wananchi kufahamu uzuri wa pamba hiyo na hilo ni jukumu la viongozi wa Ushirika Mkoani Simiyu kuitangaza Pamba hiyo ya kipekee.
Aidha, Dkt. Nawanda amewataka Viongozi wa SIMCU (2018) Ltd kuhakikisha wanashiriki na kusimamia kikamilifu zoezi la usambazaji wa Viuadudu na Vinyunyizi vya zao la pamba kwa wakulima ambalo linategemea kuanza.“Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inaratibu na kusimamia shughuli ya usambazaji na ugawaji wa dawa hizo kupitia Vyama vya Msingi ambavyo ni wanachama wa SIMCU (2018) Ltd, hatutegemei kusikia malalamiko kwa wakulima wetu na mtambue kabisa yoyote atakayeenda kinyume na maelekezo ya Serikali atachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria,” Dkt Nawanda aliongeza.
Mgeni Rasmi Dkt. Nawanda amesema Serikali imekusudia msimu 2023/2024 kuanza kutumia mfumo wa kidigitali katika upimaji na uuzaji wa zao la Pamba hivyo Viongozi wa Ushirikia wanapaswa kuanza kutoa elimu kwa wakulima kuhusu mifumo inavyotumika kuuza mazao ya wakulima ili kuwajengea wakulima uelewa kabla ya kuanza utekelezaji.
Kwa upande wake Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika - Uratibu na Uhamasishaji,Consolata Kiluma amesema kuwa ili kuwe na Vyama vya Ushirika imara na vinavyojitegemea kiuchumi na kutoa huduma stahiki kwa wanachama inapaswa Vyama vya Ushirika kujenga mitaji kwa kuwekeza katika Benki ya Ushirika ya Kitaifa inayotarajia kuanza hivi karibuni.
Aidha, Bi Consolata alisisitiza kuwa huu ni wakati wa SIMCU na AMCOS kuondokana na hati zenye mashaka za ukaguzi kwa kufanya mambo yote kwa kufuata utaratibu na maelekezo na ushauri unaotolewa na COASCO ili Vyama hivyo visiingie tena katika kundi la hati zenye mashaka.
Vile vile Naibu Mrajis alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha Viongozi wote wa Ushirika kuwa wapo kwa mujibu wa Sheria hivyo wanapaswa kusimamia na kutekeleza majukumu yeo kwa mujibu wa Sheridan ya Vyama vya Ushirika Na. 6 ya mwaka 2013 na Kanuni zake na Masharti ya Vyama hivyo na Sheria nyingine za nchi.