Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeahidi kujenga Ghala la kuhifadhia Viazi kwa  Chama cha Msingi cha Ushirika ISOWELU AMCOS kilichopo mkoani Njombe.Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Hussein Bashe ametoa ahadi  hiyo leo tarehe 17/01/2022 wakati wa kikao baina yake na wakulima na wanachama wa   ISOWELU AMCOS ambapo Chama hicho hakina ghala la kuhifadhia mazao na kusababisha wakulima kuuzia mashambani.

Waziri Bashe amesema AMCOS hiyo inapaswa kuwa ya mfano na sehemu ya kujifunzia kwa AMCOS nyingine kutokana na utendaji wake kuwa mzuri na kuonesha matokeo. “Unajua Benki kukipatia Chama cha Ushirika mkopo wa Shilingi Billion moja  inamaanisha chama hicho kiko vizuri sana katika utendaji wake na katika urejeshaji mikopo, ni vyama vichache vinaweza kuaminika kama ISOWELU AMCOS; Sasa inapaswa vyama vyote viiige mambo mazuri kama ya Ushirika huu wa ISOWELU,”  amesema Mhe. Bashe.

Waziri Bashe ameupongeza Ushirika wa ISOWELU AMCOS na kueleza wanachama wake wanalima viazi na kuvuna gunia 210 kwa ekari moja na kueleza huu ndiyo Ushirika unaohitajika nchini. Aidha, Mhe. Bashe ameagiza Vyama Vikuu vyote vya Ushirika kusajiliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) na kuwa wakala wa Mbolea ili kurahisisha huduma za upatikanaji wa Mbolea kwa wanachama wake.

Naye Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, Dkt. Benson Ndiege, ametoa rai kwa ISOWELU AMCOS kuendelea kufanya kazi ya  kuwahudumia wakulima kwa kuzingatia kanuni taratibu na sheria zinazosimamia Vyama vya Ushirika na uadilifu mkubwa.

“Mnafanya vizuri mmepata sifa nyingi na mtaendelea kupata sifa hizo sasa msilewe sifa mkaanza kufanya mambo ya ajabu mkaanza kuharibu sifa hizi ziwajenge na zisibomoe,” amesema  Dkt. Ndiege. Mrajis ameitaka ISOWELU AMCOS  kujipambanua na kujihusisha na uzalishaji wa mazao mengine na hivyo kuendelea kuboresha maisha yao baada ya mauzo badala ya kujikita kwenye kilimo cha viazi pekee.

Aidha, Mrajisi amewashauri viongozi wa Ushirika wa ISOWELU AMCOS kuendelea na mchakato wa kuwapatia wanachama wao Bima ya Afya  ili wanachama wake waweze kupata huduma za matibabu wanapougua.

Kwa upande wake Meneja wa ISOWELU AMCOS, Chesco Ng’eve, amesema Ushirika umewalea na kuwasimamia vyema ndiyo maana wamekuwa ni AMCOS bora kutokana na kusikiliza na kufuata maelekezo ya viongozi.