Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dotto Biteko amesema Serikali itaendelea kuunga mkono mageuzi chanya yanayofanyika kukuza sekta ya Ushirika.

Ameyasema hayo wakati wa akifunga Maadhimisho ya Ushirika Duniani Julai 7, 2024 katika Viwanja vya Ipuli Mkoani Tabora.

Amesema miongoni mwa hatua za mageuzi hayo ni pamoja na uanzishwaji wa Benki ya Taifa ya Ushirika ambayo itamilikiwa na wanaushirika kwa asilimia 51 inayotarajiwa kuzinduliwa karibuni.

Aidha, amepongeza uanzishwaji wa Mfuko wa Utafiti za Ushirika utakaosaidia kuibua changamoto na kuzitafutia suluhu.

Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe (Mb) amesema tayari Serikali imetoa Bil.13 ya Ruzuku kwa wakulima wa Tumbaku kwa lengo la kufidia gharama za uzalishaji na Serikali itaendelea kutoa Ruzuku kwa mazao mengine.

Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege  amesema tayari Tume imeunda na inatumia Mfumo wa TEHAMA wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (MUVU) kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa sekta ya Ushirika.

Ameeleza tayari vyama 6,319 vimesajiliwa kwenye Mfumo.

Maadhimisho hayo yamefanyika kuanzia 29 Julai, 2024 yakiambatana na makongamano pamoja na maonesho ya bidhaa na huduma za Ushirika.