Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe, amesema Serikali itaendelea kuimarisha Ushirika kwa kuongeza tija katika Kilimo kitakachochangia katika kuinua uzalishaji wa mazao na kuongeza nguvu ya Ushirika  kujiendesha kibiashara.

Mhe. Bashe amesema hayo wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani Julai 01, 2023 katika Viwanja vya Nanenane Ipuli Mjini Tabora yaliyofanyika mkoani hapo kuanzia Juni 26, 2023.

Akiongea na Wanaushirika amesema Serikali inafanya kazi kubadilisha kilimo cha Wakulima nchini ili kiweze kuwa chenye uzalishaji mkubwa wa mazao kwa kuongeza na kuimarisha miundombinu ya Kilimo hususani kilimo cha umwagiliaji hadi kufikia kiasi cha Hekari Millioni 8 ifikapo 2030. Hivyo, kuongeza uzalishaji wa mazao yatakayouzwa kupitia Ushirika utakaonufaisha wakulima kibiashara.

Aidha, amesema Serikali itaendelea kuwekeza fedha na kurasimisha Kilimo ili wakulima nchini waweze kutumia mifumo inayotambulika rasmi na kuwapa urahisi wa kufanya biashara. Akieleza baadhi ya jitihada hizo ni pamoja na kuongeza miradi zaidi ya kilimo, kuendelea kutoa ruzuku za pembejeo, vitendea kazi ambavyo muelekeo wa Serikali ni kutekeleza kupitia Vyama vya Ushirika.  

Mhe. Bashe amewataka wafanyabiashara kununua mazao ya wakulima kwa vipimo sahihi ili wakulima waweze kupata malipo sahihi yanayoendana na uzalishaji wa mazao yao. Akipongeza matumizi ya mizani ya kidijitali pamoja na Mfumo wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (MUVU), mizani hizo tayari zimeanza kutumika katika mazao ya Kahawa mkoani Kagera na Ufuta mkoani Lindi na kutoa rai mizani hizo kuendelea kutumika katika mazao mengine. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamisheni ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Abdulmajid Nsekela, amesema miongoni mwa vipaumbele vya Tume katika kuimarisha na kuongeza tija ya Ushirika Kamisheni itaendelea kusimamia mchakato wa uanzishwaji wa Benki ya Taifa ya Biashara (KCBL). Amebainisha kuwa kupitia Benki hii Vyama vya Ushirika vitanufaika na huduma mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa mikopo, Benki ambayo itamilikiwa na Wanaushirika kwa asilimia 51 na Sekta binafsi asilimia 49.

 Amesema Tume itaendelea kuvijengea uwezo vyama ili vijiendeshe kibiashara kwa kuzingatia masuala ya utoaji huduma bora, ubunifu na kujitangaza. Pamoja na mambo mengine amesema Tume itasimamia Vyama vya Ushirika kuimarisha Uwekezaji wa mali za Ushirika katika Uzalishaji ikiwemo mashamba, maghala na ujenzi wa viwanda.

Ameongeza kuwa Tume itaendelea na jitihada za kuhamasisha Ushirika kwenye Sekta mbalimbali na makundi maalum ili kuhakikisha kuwa wananchi wengi zaidi wananufaika na Mfumo wa Ushirika. Ameongeza kuwa Vyama vya Ushirika 18 vya  mazao ya bustani  vimesajiliwa na uhamasishaji unaendelea pia katika Sekta ya Madini na nyingine unaendelea.

Maadhimisho hayo yamefanyika Mkoani Tabora kwa mara ya tatu yakiwa na kauli mbiu “Ushirika kwa Maendeleo Endelevu” yakihusisha Maonesho, makongamano, michezo, kujali jamii na majadiliano mbalimbali ya kuimarisha na kuendeleza Ushirika.