Serikali imedhamiria kuimarisha benki ya Ushirika nchini

 

Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuimarisha Benki ya Ushirika Kilimanjaro (Kilimanjaro Cooperative Bank Ltd – KCBL) kwa lengo la kuwaletea maendeleo ya kweli Watanzania na kuwapunguzia umaskini.

 

Dhamira ya kuimarisha Benki ya ushirika imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya alipofungua Kongamano la Uwekezaji kwenye Benki ya Ushirika Kilimanjaro (KCBL) lililofanyika Jijini Dodoma leo tarehe 30/11/2020.

 

Amesema Serikali ya awamu ya tano, inayoongozwa na Mh. Dk. John Joseph Pombe Magufuri – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imedhamiria kwa dhati kuleta maendeleo ya kweli kwa watanzania na kuwapunguzia umaskini. Hivyo, kuimarishwa kwa KCBL kutasaidia Serikali kufikia azima yake ikiwa ni pamoja na kuimarisha huduma za jamii na kuwaongezea kipato kupitia huduma za kifedha zitakazotolewa na KCBL kwa wananchi.

 

“Serikali ya awamu ya tano inatambua umuhimu wa Ushirika nchini na ndio maana inaendelea kuweka mikakati mbalimbali ya kuimarisha shughuli za ushirika nchini ikiwemo kuchukua hatua kwa wote wanaobainika kutumia vibaya mamlaka yao pamoja na kufanya ubadhirifu kwenye Vyama vya Ushirika nchini,” amesema Bw. Kusaya.

 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo amesema kuwa kuimarika kwa Benki ya KCBL kutatoa fursa kwa Vyama vya Ushirika pamoja na wananchi kwa ujumla kupata huduma za Kifedha kwa karibu zaidi. Amewahamasisha wanaushirika wote pamoja na wadau mbalimbali kutumia fursa hii ya uwepo wa KCBL kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa huduma za kifedha nchini.

“Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania pamoja na Benki Kuu ya Tanzania, vitaendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwenye Benki hii na kuhakikisha Benki inasimama na kutoa huduma zinazokusudiwa,” amesema Katibu Mkuu.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dkt. Anna Mgwira, amewataka Wanaushirika, Mashirika na Watu binafsi kushirikiana kuanzisha na kuendeleza Benki ya Ushirika ya kitaifa nchini kwa lengo la kumkomboa Mwananchi na Mwanaushirika.

“Tushikamane kuanzisha na kuendeleza Benki ya Ushirika ya kitaifa, tuwakomboe wananchi wetu na ninawaomba kila mmoja wetu awekeze katika benki hii, iwe chama cha ushirika, mtu binafsi au mashirika,” amesema Dkt. Mgwira.

Akizungumza katika Kongamaono hilo, Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, amesema Benki ya KCBL inapaswa kuendeshwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha pamoja na Kanuni zake na inapaswa pia kuzingatia matakwa ya Sheria ya Vyama vya Ushirika Na.6 ya Mwaka 2013 pamoja na Kanuni zake kwa lengo la kutekeleza matakwa ya Sheria husika.

 

“Benki hii inapaswa kutekeleza Sheria nyingine mbalimbali za nchi ili kuepuka ukiukwaji wa Sheria zinazotakiwa kutekelezwa kwa mujibu wa shughuli zinazoendeshwa na Benki,” amesema Dkt. Ndiege.

 

Mrajis amesema Benki ya KCBL imekuwa ikitoa huduma za Kifedha kwa wananchi wengi waliopo Mkoani Kilimanjaro na baadhi ya maeneo katika mkoa wa Tanga pamoja na Vyama vingi vya Ushirika kwa kipindi kirefu na imesaidia sana Vyama hivyo kupata huduma za kifedha kwa kuzingatia uwezo wa vyama na kuwekwa kwa masharti ambayo yaliendana na uwezo wa Vyama hivyo.

 

Awali akiongea katika Kongamano hilo, Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya KCBL, Dkt. Gervas Machimu, amesema Nguvu ya ushirika ni umoja wetu na amewataka washiriki wa kongamano hilo kuwa tayari kumiliki benki pekee ya ushirika nchini (Coop Bank of Tanzania).

“Kwa pamoja, na kwa kushirikiana na watu binafsi, makumpuni, taasisi za umma na masoko ya mitaji, tumedhamiria kuijenga upya benki ya KCBL kimuundo, kimtaji na usimamizi ili iwe benki kubwa na kishika bendera kwa vyama vyote vya ushirika nchini kwa mahitaji yao ya kifedha,” mesema Dkt. Machimu.